Wadaiwa sugu kodi ya ardhi waonywa

KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Allan Kijazi, amewataka wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi kulipa kodi kabla serikali haijaanza kuwachukulia hatua za kisheria.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao kazi kati ya Benki ya CRDB na wasimamizi wa kodi wa Wizara ya Ardhi kutoka mikoa yote nchini leo, Novemba 4, 2022 mjini Arusha, alisema watakaokaidi agizo hilo wako hatarini kupoteza milki ya ardhi zao.

“Suala la kulipa kodi ya ardhi ni la kisheria ni vyema wananchi wote wakazingatia matakwa ya kisheria kwa kulipa kodi hiyo…Serikali imetoa msamaha wa riba kwa walipa kodi sugu na mwisho wa msamaha huo ni Desemba mwaka huu,” alisema Dk Kijazi.

Akielezea zaidi alisema madeni ya kodi ya ardhi ni takribani Sh Bil.70 na kusisitiza kuwa hata kama msamaha wa riba ya kodi ya ardhi utakoma Desemba mwaka huu, bado wataendelea kudai malimbikizo ya kodi ya ardhi kwa wale watakaoendelea na kumilki ardhi bila kulipa kodi.

Alizisisitiza taasisi za umma kuona haja ya kulipa kodi ya pango la ardhi, kwani malimbikizo hayo yanazihusisha pia ikiwemo na taasisi binafsi, huku akisema uzoefu unaonesha kiwango kinachokusanywa ni kidogo kulinganisha na uhalisia kwa idadi ya walipa kodi.

Habari Zifananazo

Back to top button