Wadaiwa wapewa siku 14 kurejesha mikopo

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Tambaza Auction Mart na General Brokers Limited, kwa niaba ya Bodi ya Amana, imetoa siku 14 kwa wadaiwa sugu pamoja na wadhamini wao kuhakikisha wanarejesha mikopo yao kabla ya hatua kali za kisheria kuchukuliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni16,2025 jijini Dar es Salaam , Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Abdallah Abed, amesema lengo la serikali kuruhusu taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa wananchi ni kuwawezesha kutimiza malengo yao ya kiuchumi. Hata hivyo, alieleza kuwa kutorejeshwa kwa mikopo hiyo kumesababisha baadhi ya benki kufilisika.
“Natoa wito kwa wote waliokopa kupitia benki ya FBME, Covenant for Women pamoja na Efatha, kuhakikisha wanarejesha fedha hizo mara moja. Mikopo hii ni kwa ajili ya kuwanufaisha wengi, na kuchelewesha au kutolipa kabisa kunapora fursa kwa wengine wenye uhitaji,” amesema Abed.
Ameongeza kuwa, benki ya Efatha peke yake inadai zaidi ya Sh bilioni 5 kutoka kwa wadaiwa mbalimbali, jambo linaloathiri ustawi wa taasisi hiyo.
“Fedha hizi ni nyingi sana. Tunatoa rai kwa wadaiwa walioweka dhamana kuhakikisha wanamaliza madeni yao. Iwapo dhamana zitaonekana hazitoshi, tutachukua mali nyingine kwa mujibu wa sheria. Pia, endapo mdaiwa amefariki dunia, mzigo huu utahamia kwa mdhamini wake,” anasisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni wa Kampuni hiyo, Sabrina Abeid amesema zaidi ya watu 500 wanadaiwa na wamehusika moja kwa moja katika kusababisha baadhi ya benki kufungwa kutokana na kutorejesha mikopo.
“Sasa hivi tuna mifumo ya kisasa ya kuwafuatilia wadaiwa wote. Hakuna atakayesalimika. Tunawahimiza wajitokeze mapema kabla hatua zaidi hazijachukuliwa,” amesema.
Naye Mkuu wa Usalama wa Tambaza Auction Mart, Omary Thamsy anaeleza kuwa hakuna mchezo katika kutekeleza operesheni hiyo, na kuwataka wahusika kufika katika jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya kuhakiki taarifa zao.
“Taarifa hizi zimekuwa zikitolewa mara kwa mara kupitia magazeti na vyombo vya habari lakini bado kuna watu hawazichukulii kwa uzito. Tunawaonya, safari hii hatutasita kuchukua hatua,” amesema.
Anatoa wito kwa serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu mikopo, ili jamii ielewe kuwa fedha wanazopewa si msaada bali mkopo unaopaswa kurejeshwa kwa wakati.
“Watu wengi wanachukulia fedha hizi kama zawadi. Huo ni mtazamo potofu. Elimu ya mikopo inahitajika sana ili kujenga utamaduni wa uwajibikaji na kusaidia mzunguko wa fedha kwenye jamii,” amesema.