Wadau: Marekebisho sheria za uchaguzi yaonesha uongozi bora

WADAU wa masuala ya siasa wamesema marekebisho ya sheria za uchaguzi yameondoa kero, kurejesha matumaini kwa wapigakura na kuonesha uongozi bora wa serikali iliyopo madarakani.
Walisema hapo nyuma kilio kikubwa kilikuwa katika sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi kuwa hazikuwa rafiki hasa kwa vyama vya upinzani.
Akizungumza na HabariLEO Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT), Dk Dotto Bulendu alisema marekebisho ya sheria yaliyofanyika yanaipa uwezo Tanzania kuendesha uchaguzi wa huru na haki pamoja na kurudisha imani kwa wananchi kushiriki katika uchaguzi ujao.
“Marekebisho haya yana umuhimu mkubwa hasa katika kurudisha hamasa ya watu kupiga kura na kujitokeza kugombea kwa sababu wana imani kuwa sasa uwazi umeongezeka,” alisema Dk Bulendu.
Mwaka 2022 kupitia kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau kuhusu demokrasia na vyama vingi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kilipendekeza maoni kadhaa juu ya mabadiliko ya mfumo wa kisheria hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Kupitia mapendekezo hayo, Bunge la Tanzania mwaka 2024 lilitunga sheria mbili muhimu, moja ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya 2024.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulkarim Atiki alisema marekebisho yaliyofanyika yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mkono wa serikali katika shughuli za uchaguzi.
“Ukizingatia kulikuwa na malalamiko yaliyotoka kwa vyama vya siasa wakidai tume ina kasoro na sheria na kanuni Rais Samia alifanya mashauriano na vyama kupitia kikosikazi na kuleta mabadiliko ya sheria za uchaguzi,” alisema.
Aidha Dk Bulendu alisema malalamiko na kero nyingi zilizotolewa na vyama vya siasa zimefanyiwa kazi kupitia sheria hizo na kuonesha uongozi uliopo madarakani unasikiliza matakwa ya watu na kuyatekeleza.
“Kilio kikubwa kilichokuwa kinapigiwa kelele na sasa kimefanyiwa kazi kuondoa mamlaka ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi maana walionekana kama makada na walikuwa hawatendi haki,” alisema.
Aliongeza: “Na hii ndio kero kubwa, kitendo cha kuwaondoa na maofisa waandamizi kusimamia uchaguzi kunaleta uwanja rafiki wa kupiga kura na serikali kusiliza matakwa ya upinzani ni ishara ya uongozi bora.”
Mabadiliko mengine ni juu ya mawakala kuruhusiwa kushuhudia uchaguzi, wadau hao walisema kitendo cha mawakala kushuhudia upigaji kura na kuhesabu kura kunaongeza uwazi, hivyo kutoa nafasi wagombea wote kushuhudia na kupunguza malalamiko na itaongeza idadi ya wapigakura katika uchaguzi wa Oktoba.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari alisema serikali imekuwa sikivu kwa kuitikia matakwa ya vyama vya upinzani na kufanya marekebisho hayo.
“Chimbuko la mabadiliko ya sheria tuliyofanya yalikuwa ni mapendekezo ya vyama vya siasa kupitia kikosi kazi maalumu kilichoongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala,” alisema.
Kadhalika utaratibu wa kuwapata wajumbe wa tume watakaopatikana kwa njia ya usaili uliungwa mkono na wadau hao, walisema itaongeza uwazi na uwajibikaji kwa wasimamizi wa uchaguzi.