WADAU wa elimu na wananchi mbalimbali wameombwa kuhudhuria kongamano la tatu la kitaifa la huduma za maktaba, tamasha la vitabu na usomaji.
Kongamano hilo limeanza leo Septemba 19, 2023 na linatarajia kuisha Septemba 21 mwaka huu katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) jijini Mwanza.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania(TLSB) Dk Mboni Ruzegea wakati wa mahojiano malumu na HabariLEO.
Dk Ruzegea amesema lengo kuu la kongamano hilo ni kutoa fursa kwa wadau wote wa huduma za maktaba nchini kushiriki, kujadili, kuchangia na kuamua kwa pamoja upatikanaji na utumiaji wa huduma bunifu za maktaba na teknolojia za kisasa nchini kunavyosaidia kujenga ari na utamaduni wa kujisomea.
Amesema mada kuu ni kukuza vipaji vya uandishi na uchapishaji,kujenga ari na utamaduni wa kujisomea kupitia huduma bunifu za maktaba.
Amesema kongamano hilo kutakuwa na mafunzo ya ukutubi na uhifadhi Nyaraka kwa wakutubi na watunza nyaraka na habari kutoka wizara, idara na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wa kutoa huduma bora za maktaba na habari kwa njia za kidijitali.
Mkurugenzi wa uendeshaji huduma za maktaba wa Bodi ya Huduma za Maktaba (TLSB) Dk Rehema Ndumbaro amewaomba Watanzania kujiwekea utaratibu wa kujisomea vitabu na machapisho mbalimbali ili kuongeza uelewa wa mambo mbalimbali.