Wadau wa kodi wataka haki mizozo na TRA

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda.

MFUMO wa kodi nchini Tanzania una kazi kubwa kufadhili huduma za umma na maendeleo yakiwamo ya miundombinu nchini.

Pamoja na umuhimu huo, Tanzania inakabiliwa na changamoto za kiusimamizi zinazokwamisha ufanisi katika ukusanyaji wa kodi.

Masuala yanayohusu utekelezaji wa kanuni na sheria za kodi, ugumu katika usimamizi wa utekelezaji na wigo finyu wa vyanzo vya kodi ni miongoni mwa mambo makubwa yanayodhoofisha mfumo.

Advertisement

Aidha, uwepo wa taasisi nyingi ambazo ni kama wakala wa ukusanyaji huku kila moja ikiwajibika kwa kodi tofauti, hujenga mazingira yaliyogawanyika na hupunguza ufanisi na kuwachanganya walipa kodi.

Makala haya yanajikita kutazama kwa kina changamoto hizi yakijumuisha takwimu halisi, mifano hai kutoka kanda na mabara mengine pamoja na mapendekezo yanayotolewa na umma kuhusu maboresho.

Yanaangalia kwa kina pia namna mkakati unavyohusisha masuala ya kielektroniki (kidijiti), uwazi na namna mbinu ya pamoja inavyoweza kuchochea utekelezaji wa sheria za kodi na kuweka mfumo imara zaidi wa mapato.

Usimamizi wa kodi
Mtaalamu wa kodi kutoka Bagamoyo mkoani Pwani, Badra Omar anazungumzia udhaifu uliopo katika mfumo wa kodi nchini. Kwa mujibu wa Omar, wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiwa na jukumu kuu la ukusanyaji
kodi ikisimamia kodi ya mapato ya mashirika, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ushuru wa forodha na kodi ya bidhaa, haifanyi kazi peke yake.

Badala yake, TRA inafanya kazi ndani ya mfumo wa usimamizi wa kodi uliogawanyika sana kwa kuwa zaidi ya taasisi 60 tofauti zikiwemo mamlaka za serikali za mitaa, vyombo vya udhibiti kama Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) navyo hutoza na kukusanya kodi, tozo na ada mbalimbali.

Omar anasema uwepo aasisi nyingi zinazokusanya kodi kama wakala umezua uzembe na kusababisha kuwapo mwingiliano wa majukumu ya kodi, kuwapo kwa hatua nyingi zisizohitajika katika utekelezaji wa sheria za kodi na hata kuongezeka kwa gharama za usimamizi katika biashara.

Hali hii ya kusimamia madai ya kodi kutoka katika taasisi mbalimbali mara nyingi husababisha mkanganyiko hasa kwa biashara ndogo na za kati (SMEs) na kupunguza ari ya kulipa kodi kwa hiari. Anasema upungufu huu
hudhihirika katika uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa ambao mwaka 2023 ulikuwa asilimia 11.9 chini ya wastani wa kikanda wa asilimia 16 katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Upungufu huu unadhihirisha matokeo ya mfumo tata wa kodi ambao si tu kwamba unakwamisha juhudi za kurasimisha biashara, bali pia unazuia uwezo wa serikali kupanua wigo wa vyanzo vya kodi. Kwa mujibu wa Omar,
ili kukabili changamoto hizi hapana budi kuwapo mfumo wa pamoja wa usimamizi wa kodi ulioratibiwa vyema zaidi.

Kimsingi kurahisisha juhudi za ukusanyaji kodi chini ya taasisi chache zilizounganishwa na kuratibiwa sawia, kutapunguza uwepo wa taasisi ambazo si za lazima wala muhimu, kutaongeza ufanisi na kutajenga mazingira rafiki
ya biashara.

Anasema maboresho hayo hatimaye yataongeza mapato ya umma huku yakipunguza mzigo wa urasimu kwa mashirika na kampuni za biashara, hivyo kuimarisha mfumo wa kodi wenye usawa na ufanisi .

Changamoto za mfumo wa ulipaji kodi
Mhasibu wa Kampuni ya Kiwelu Associates ya mjini Moshi, Kelvin Kiwelu anasema ulipaji mdogo wa kodi bado ni moja ya changamoto kuu zinazokabili usimamizi wa kodi Tanzania. Anasema sekta isiyo rasmi inayochangia takribani asilimia 50 ya pato la taifa kwa kiasi kikubwa iko nje ya mfumo rasmi wa kodi, hivyo kuwa kikwazo
kikubwa katika ukusanyaji wa mapato.

Kutokana na hali hii biashara nyingi katika sekta isiyo rasmi ama zinashindwa kujisajili TRA, au zinapuuza au
kuzembea kuwasilisha taarifa kuhusu ulipaji kodi.

Kwa mujibu wa Kiwelu, hali hii ya kukithiri kwa biashara nyingi kutolipa kodi kwa mujibu wa sheria inachangiwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwapo taratibu ngumu za usajili na uwasilishaji taarifa kuhusu kodi, kukosekana miongozo ya kutosha kutoka mamlaka za kodi na hofu ya viwango vya juu vya kodi.

Anasema amejionea hali hiyo Moshi, lakini anaamini ni suala la nchi nzima. Anasema changamoto hii inachochewa na kuwapo mgawanyiko katika ukusanyaji kodi hali inayosababisha kila wakala kuweka kanuni zake, makataa
(muda wa mwisho wa malipo) pamoja na mifumo ya kodi.

Kukosekana kwa mfumo mmoja kunachanganya walipa kodi na kuweka mazingira yanayosukuma wafanyabiashara  kuona kuwa, kutokulipa kodi ndiko chaguo sahihi hali inayofanya biashara ndogo na za kati kubaki nje ya mfumo
rasmi. Hali hii si ya Tanzania pekee.

Kwa mujibu wa Kiwelu, tafiti za kimataifa zinaonesha kuwa nchi zenye mifumo rahisi ya kodi huwa na viwango vya
juu vya ulipaji kodi.

Kwa mfano, maboresho ya kodi yaliyofanyika Rwanda yakilenga kurahisisha taratibu na kuweka kodi kidijiti yamesababisha ongezeko kubwa la utekelezaji wa sheria na ulipaji kodi huku uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa ukipanda hadi takribani asilimia 16 katika miaka ya hivi karibuni pamoja na zaidi ya asilimia 11.9 ya Tanzania kama ilivyorekodiwa mwaka 2023.

Aidha, nchi kama Estonia ambazo zimetumia mifumo kamili ya kodi ya kidijitii yenye vikwazo vidogo vya urasimu
zinaripoti kuwapo zaidi ya asilimia 95 ya viwango vya ulipaji kodi. Akitumia mifano hiyo, Kiwelu anasisitiza kuwa Tanzania haina budi kurahisisha usimamizi wake wa kodi, kuunganisha wakala zinazoingiliana pamoja na kuanzisha mfumo unaofikika na wa uwazi zaidi.

Anasema majukwaa ya kidijiti, mipango ya wazi ya elimu kwa mlipakodi pamoja na kupunguzwa kwa urasimu
kutachochea biashara zaidi hususani katika sekta isiyo rasmi kutekeleza wajibu katika ulipaji kodi na hivyo, kupanua
wigo wa vyanzo vya kodi na kuongeza mapato ya serikali.

Ulipaji kodi
Mwanauchumi aliyeko Mombasa nchini Kenya, Warda Hussein anasema bado utekelezaji wa kodi ni changamoto kubwa katika mfumo wa kodi nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Anasema kuwapo kwa rasilimali chache, mbinu za kizamani za ufuatiliaji na hata uratibu usio na tija miongoni mwa mashirika mbalimbali yanayokusanya kodi unazuia ufuatiliaji na ukusanyaji wa kodi na kusababisha ongezeko la ukwepaji kodi.

Anazungumzia uzoefu wake huko Mombasa namna maeneo ya vijijini na katika masoko yasiyo rasmi yanavyoathirika kutokana na mifumo dhaifu inayoweka urahisi kwa wafanyabiashara kukwepa kodi.

Kwa mujibu wa Hussein, hali kama hiyo ndio inayoikumba Tanzania, ambapo juhudi zisizo za pamoja katika
utekelezaji wa pamoja na vitendo vya rushwa zinachangia kukosekana kwa ufanisi katika ukusanyaji wa kodi.

Ripoti ya Mitazamo Kuhusu Rushwa ya Mwaka 2023 inabainisha kuwa, Tanzania inaendelea kukabiliana na vitendo vya rushwa ndani ya usimamizi wake wa kodi huku mambo hayo yakiondoa uwajibikaji na imani ya wananchi katika mfumo huo.

Rushwa, upendeleo na ukosefu wa uwazi katika utekelezaji wa matakwa ya kodi unaruhusu biashara zisizotekeleza kanuni na sheria za kodi kuendelea kukwepa jukumu, na hivyo kudhoofisha juhudi za ukusanyaji mapato. Miongoni mwa masuala yanayosumbua zaidi ni ukosefu wa mkakati wa utekelezaji wa pamoja hali inayosababisha matumizi ya adhabu yasiyo sawa kwa wasiolipa kodi.

Baadhi ya biashara hukabiliwa na athari mbaya huku nyingine zikikwepa kodi bila athari yoyote au kupata athari
kidogo hali inayofifisha athari za kuzuia vikwazo vya kisheria. Kwa mujibu wa Hussein, mtindo huu si wa Tanzania
pekee kwani nchi nyingi zinazoinukia kiuchumi zinakabiliwa na changamoto zinazofanana za utekelezaji kutokana na uwezo dhaifu wa kitaasisi na udhaifu katika usimamizi.

Hata hivyo, miundo iliyofaulu kutoka mikoa mingine inaonesha kuwa changamoto za utekelezaji zinaweza kushindwa kupitia maboresho yanayosukumwa na teknolojia. Kwa mfano, Korea Kusini imetumia vyema teknolojia ya kidijiti kuboresha ufuatiliaji na utekelezaji wa kodi, hivyo kusababisha viwango vya juu zaidi vya ulipaji kodi na hivyo kuondoa kuvuja kwa mapato.

Nchi imetekeleza tathmini za viashiria vya hatari vinavyotokana na matumizi ya akili mnemba (AI), ufuatiliaji wa miamala kwa wakati halisi pamoja na mifumo ya kidijiti ya kuripoti inayopunguza au kuzuia rushwa na watu kuingilia huku ikiongeza ufanisi.

Hussein anasema Tanzania inaweza kuimarisha mfumo wake wa ulipaji kodi kwa kutumia ufumbuzi wa kidijiti
kama huo. Hii ni pamoja na kanzidata ya pamoja ya vyanzo vya kodi, ufuatiliaji wa kielektroniki na mifumo ya kugundua ulaghai inayoendeshwa na akili mnemba.

Kwa kuimarisha miundombinu ya kiteknolojia na kuhakikisha kuwa uwazi zaidi katika ulipaji kodi, Tanzania  inaweza kuongeza viwango ulipaji kodi, kuzuia rushwa na kuongeza ukusanyaji wa mapato na hivyo, kuweka mfumo wa kodi wenye ufanisi na usawa zaidi.

Tofauti katika ukusanyaji mapato
Mshauri wa Masuala ya Fedha aishiye Sumbawanga, Joshua Kabigi anasema mapato ya kodi nchini yanakita zaidi kwa mashirika makubwa ambayo ni machache hasa katika sekta ya mawasiliano ya simu, benki na katika sekta ya uziduaji.

Utegemezi huu mkubwa kwa walipa kodi wakuu wachache unaiweka nchi katika hatari za kiuchumi, kwani kushuka kwa kuwa mabadiliko katika sekta hizi yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato kwa ujumla.
Kwa mujibu wa takwimu za TRA, zaidi ya asilimia 70 ya mapato ya kodi yanazalishwa na chini ya asilimia 10 vyanzo vya kodi villivyosajiliwa.

Kukosekana huku kwa uwiano kunaacha sehemu kubwa ya uchumi hasa katika biashara ndogo na za kati na sekta isiyo rasmi kwani zinachangia kwa kiasi kidogo katika mapato ya kodi, licha ya nafasi yao kuwa kubwa katika ajira na shughuli za kiuchumi.

Tatizo linachochewa zaidi na mfumo uliogawanyika wa kukusanya kodi unaoweka viwango vingi vya kodi, michakato migumu ya usajili na kukosekana usimamizi maalumu katika mashirika (wakala) mbalimbali. Upungufu huu unakwamisha biashara zisizo rasmi na zinazoibukia kurasimisha na hivyo, kuzuia ongezeko la vyanzo vya
kodi.

Kwa mujibu wa Kabigi, nchi zenye mifumo jumuishi na rahisi zaidi ya kodi zimefanikiwa kupanua wigo wa vyanzo vya kodi na kuimarisha ustahimilivu wa kifedha.

Kwa mfano, maboresho ya kodi nchini Rwanda yaliyolenga katika mfumo wa kidijiti, kurahisisha usajili na kuboresha elimu ya mlipakodi, yamesababisha kuwapo uwiano wa juu wa kodi kwa Pato la Taifa wa takribani asilimia 16 ikilinganishwa na asilimia 11.9 ya Tanzania mwaka 2023.

Nchi ya Mauritius pia imejenga msingi thabiti na tofauti wa kodi kwa kurahisisha taratibu za kodi na kuunganisha
teknolojia katika usimamizi wa kodi ili kuhakikisha biashara nyingi zinatekeleza kanuni na sheria za kodi bila kuwapo utitiri wa vikwazo vya ukiritimba.

Kabigi anasisitiza kuwa, ili kupunguza utegemezi huu katika kundi dogo la mashirika makubwa na kuleta utulivu wa
vyanzo vya mapato, Tanzania inapaswa kutekeleza maboresho yaliyolengwa ili kuchochea ulipaji kodi miongoni mwa biashara ndogo na za kati na sekta isiyo rasmi.

Maboresho haya ni pamoja na kurahisisha hatua za usajili wa kodi, kuunganisha mashirika au wakala wa kukusanya kodi na kutumia mifumo ya kidijiti (kielektroniki) kurahisisha michakato ya malipo ya kodi. Kwa kupanua wigo wa vyanzo vya kodi, Tanzania itapunguza hatari zinazohusu mabadiliko ya uchumi katika sekta muhimu na kuunda mfumo wa kodi ambao ni wa usawa na endelevu.

Sheria na sera
Mbunge maarufu anayekataa jina lake lisiandiukwe gazeti, anasema mabadiliko ya mara kwa mara katika sheria za kodi na utata wa kanuni zilizopo ni vikwazo vikubwa kwa walipa kodi nchini.

Anasema changamoto hizi za kisheria, matumizi yanayotofautiana ya sheria za kodi na kutokuwapo kwa mfumo wa pamoja wa usimamizi wa kodi ni mambo ambayo mara nyingi husababisha ulipaji duni wa kodi.

Katika maeneo mengi hususani vijijini, biashara zinajitahidi kuendana na kasi ya mabadiliko ya udhibiti na kusababisha makosa ya uwasilishaji wa taarifa za hali inayofanya biashara hizo kupata adhabu (faini).

Katika jimbo moja la uchaguzi nchini, wafanyabiashara wanadai kukabiliwa na matatizo makubwa katika kuzingatia kanuni kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara jambo linalowaweka walipa kodi katika mazingira magumu ya adhabu (faini) kutokana na kukosekana kwa uwazi (ufafanuzi).

Wingi wa mamlaka za kodi nao unatajwa kuchanganya mambo zaidi. Walipakodi hupokea taarifa na tarehe za mwisho zinazokinzana kutoka mashirika mbalimbali jambo linalosababishia mkanganyiko na kuwaongezea mzigo.

Mgawanyiko huu wa kimfumo husababisha ugumu kwa biashara kuendelea kutekeleza sheria na matakwa ya kodi hasa biashara ndogo na za kati.

Tofauti na hiyo, nchi zenye mifumo ya sheria iliyoboreshwa zikiwamo Singapore na New Zealand zimedhihirisha kuwa, kurahisisha na kufafanua sheria za kodi huchochea utekelezaji wa sheria na matakwa ya kodi na kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usimamizi.

Mataifa haya yamepitisha sera za kodi zilizo wazi zaidi na thabiti hivyo kuchochea mazingira yanayowezesha biashara zenyewe kutambua na kuzingatia wajibu wa kulipa kodi.

Mbunge huyo anasema Tanzania inaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa kwa kuoanisha sera zake za kodi na kanuni bora za kimataifa zikiwamo zinazopendekezwa na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD).

Maboresho si tu kwamba yataboresha viwango vya ulipaji kodi, bali pia yatasaidia kupunguza ukwepaji wa kodi na hata kuziba mianya ya rushwa. Mazingira wazi na thabiti zaidi ya udhibiti yatawapa wafanyabiashara utulivu unaohitajika kuwekeza, kukua na kuchangia katika vyanzo rasmi vya kodi na hivyo, kuimarisha uchumi wa
nchi.

Marekebisho yanayopendekezwa
Kutokana na changamoto nyingi zinazokabili mfumo wa kodi nchini Tanzania, wasomaji mbalimbali wakiwamo wanadiaspora wamewasilisha mapendekezo muhimu wanayotamani Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi izingatie kama sehemu ya mapitio yake yanayoendelea.

Mapendekezo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na jumuiya ya kimataifa, yanaaksi nia ya pamoja ya maboresho makubwa kuimarisha ulipaji kodi, ufanisi katika usimamizi pamoja na uwazi katika mfumo. Mojawapo ya mapendekezo maarufu yaliyotolewa na wasomaji kadhaa, ni ujumuishaji katika ukusanyaji wa kodi chini ya mfumo wa pamoja.

Kwa mujibu wa maoni ya mengi, hatua hii itasaidia kuboresha uratibu kati ya mashirika mbalimbali yanayohusika katika ukusanyaji wa kodi. Kimsingi, mbinu inayotumika sasa ambayo si ya pamoja mara nyingi husababisha mkanganyiko kwa walipakodi kwa kuwa biashara zinalazimika kwenda katika mashirika mengi yenye kanuni na
muda tofauti wa uko wa malipo unaokinzana.

Wasomaji wanasema kuweka pamoja juhudi hizi kutarahisisha taratibu za kufuata na kufanya iwe rahisi kwa biashara kuzingatia wajibu wa kulipa kodi. Kipengele muhimu katika maboresho yanayopendekezwa ni utekelezaji wa mfumo rasmi wa taarifa kwa muda wa mwisho wa kodi.

Wasomaji wengi hasa wa vijijini na wafanyabiashara wadogo wanasisitiza umuhimu wa TRA kutuma taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi katika simu (SMS) barua pepe au barua rasmi angalau siku 30 kabla ya tarehe za mwisho za pingamizi, rufaa au mawasilisho ya kodi.

Wanaamini mbinu hii itawapa walipakodi muda wa kutosha kujiandaa na kuepuka kutotekeleza matakwa, kanuni na sheria za kodi bila kukusudia. Aidha, wanapendekeza pia kuwepo lango la kidijiti ambapo walipakodi wanaweza kufuatilia muda wa mwisho na kufuatilia maendeleo ya kesi zao ili kukuza uwazi na kuboresha uwajibikaji wa umma katika usimamizi wa kodi.

Wachangiaji kadhaa ambao majina yapo hayakupatikana wanapendekeza kuanzishwa upendeleo kwa walipakodi katika kesi ambapo TRA itashindwa kujibu au kuitikia ndani ya muda unaotakiwa kisheria.

Wanaamini maboresho haya yatahakikisha ucheleweshaji unaofanywa na TRA hauwanyimi walipakodi haki hivyo kuizuia TRA kutumia ucheleweshaji wa ukiritimba kama mkakati wa kulazimisha uamuzi wa moja kwa moja kwa kujipendelea.

Msomaji mmoja kutoka ughaibuni anasema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha walipakodi wanatendewa kwa usawa zaidi. Wanatoa wito kuanzishwa kwa utaratibu wa kusuluhisha mizozo ya kodi isiyoegemea upande wowote
na kwa uhuru.

Wachangiaji kutoka mikoa mbalimbali wanaeleza haja ya kuwa na mahakama maalumu ya kodi kushughulikia mizozo bila upendeleo na hivyo kupunguza uwezekano wa uamuzi wa upande mmoja wa TRA.

Aidha, wanasema walipakodi wanapaswa kupata ushauri wa kisheria bila malipo wanapopinga uamuzi wa TRA kama mifumo iliyopo nchini Canada na Uingereza ambapo mahakama huru zimeboresha imani ya walipakodi katika mfumo.

Kuhusu rufaa, wengi wanasema muda wa miezi sita kukata rufaa mara nyingi ni mgumu na unapaswa kuwa rahisi zaidi. Wanapendekeza kuanzishwa utaratibu wa nyongeza ya muda kwa sababu zenye mashiko kama vile ugonjwa, ucheleweshaji kutokana na taratibu au ukosefu wa taarifa sahihi.

Jukumu la kuthibitisha kuwa mlipakodi alipewa taarifa sahihi na za kutosha linapaswa kuwa la TRA ilikuhakikisha rufaa hazikatazwi kwa misingi ya kiufundi katika kesi ambapo mlipakodi hakujulishwa ipasavyo. Kimsingi, wasomaji wanasisitiza mfumo wa kodi kuwekwa kidijiti.

Wanapendekeza usuluhishaji wote wa mizozo ya kodi uingizwe katika mfumo wa mtandaoni unaoweza kufikiwa na umma na kuruhusu walipa kodi kufuatilia maendeleo ya kesi zao huku pia ukiongeza uwazi. Upatikanaji wa kumbukumbu za mizozo mikubwa ya kodi kwa umma pia utaifanya TRA na mashirika mengine yanayohusika katika ukusanyaji kodi kuwajibika, kupunguza rushwa na kuongeza uadilifu wa ujumla katika mfumo wa kodi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *