Wadau wa korosho Afrika wakutana Mtwara

MTWARA; WATALAAMU na wadau wa korosho kutoka nchi nane barani AfriKa leo wamekutana Mkoani Mtwara, kujadili changamoto na fursa kwenye mnyororo wa thamani la zao la korosho nchini, AfriKa na mabara mengine duniani.
Mkutano huo utafanyika kwa siku tano mkoani Mtwara, unafanyika kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki, Tanzania ikiwa mwenyeji, umeandaliwa na Taasisi ya African Cashew Alliance (ACA) wakishirikiana na Bodi ya Korosho Nchini (CBT).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mkurungezi wa CBT, Alfred Francis amezitaja nchi zinazoshriki kuwa ni Sudan Kusini, Zambia, Msumbiji, Uganda, Rwanda, Malawi , Kenya na Tanzania.
Amesema lengo ni kuwawezesha washiriki kubadilishana uzoefu, changamoto na mafanikio kwenye masuala ya korosho.
“Lakini pia washiriki kutoka nchi zingine watajifunza kutoka kwetu hasa kwenye suala la ubora ambapo Tanzania inafanya vizuri sana, kwenye suala la utafiti, sisi tunafanya vizuri kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI),” amesema.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amemshukuru Waziri wa Kilimo na CBT kwa juhudi za kukuza sekta ya korosho nchini.
“Tunashukuru Waziri wa Kilimo na Bodi ya korosho kuwezesha kuona haya yanatokea (mkutano) ni kwa sababu ya kazi kubwa ambayo Raisi anafanya kwenye sekta hii,” amesema.
Amewaambia washiriki wa mkutano kuwa Rais Dk Samia Hassan Suluhu amefanya kazi kubwa ya kukuza tasnia ya korosho kwa kuongeza maofisa ugani, kutoa pembejeo, kutafuta masoko na kuleta wawekezaji na kuleta tija kwenye zao la korosho.