Wadau wafafanua maendeleo sekta ya bandari
MKURUGENZI wa Mipango Mamlaka ya Bandari (TPA) Dk Boniphace Nobeji amesema hadi kufikia Juni 2022 bandari zilihudumia shehena milioni 20.5 kati ya hizo zilizohudumiwa Bandari ya Dar es Salaam ni milioni 18.
Akizungumza leo katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao na kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo, Dk Nobeji amesema kwa kutambua hilo kuna haja ya kuboresha huduma za kibandari kwa ujumla wake.
“Serikali kwa miaka yote imeendelea kuwekeza kuhakikisha inaboresha huduma hizi.” Amesema Dk Nobeji.
Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bandari Kavu, Meleck Shange amesema mpaka sasa kuna bandari kavu 14 za makasha, ambayo ni makasha yenye mizigo sio matupu, na bado nyingi zinazidiwa na mzigo.
Amesema imani yake kubwa muwekezaji atavutia meli nyingi kuja Dar es salaam hivyo na wao kupata kazi kubwa zaidi.
“Ukiangalia uwekezaji ambao unafanyika sasa bandarini tunategemea hata namba ya bandari kavu ambazo tunazo utaongezeka.” Meleck Shange amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakala wa Meli (TASAA), Daniel Mallongo amesema bandari hiyo lazima iwe na magati ya kutosha meli zisikae nje, ili kuepuka gharama kubwa hivyo lazima kuwe na magati kila wakati
“Ili tuweze kuongeza shehena kwenye bandari zetu za Dar es salaam ni lazima wenye meli wawe tayari kuja katika bandari zetu.” Daniel Mallongo.” Amesema.
Mfanyabiashara maarufu Azim Dewji amesema Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa bandari sio ya watanzania pekee, Tanzania inamiliki ila inasaidia nchi saba, kwahiyo kuna biashara kubwa ambayo inaweza ikafanyika.”
“Mkataba ni biashara, ukishaweka wazi mwingine atakuja kujaza nafasi, kwahiyo serikali isiwe wazi sana, tunapaswa kuwaamini viongozi wetu.”ameeleza Dewji.
Mkurugenzi Mtendaji kutoka KC Global Links, Chris Lukosi ameishukuru serikali kwa kuingia kwenye mazungumzo na muwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam.
“Kwanza naishukuru serikali kwa kuingia kwenye mazungumzo ya kupata huu uwekezaji, kwa sababu sio mara ya kwanza tumekuwa na muwekezaji kwenye bandari ya Dar es salaam, mpaka sasa hivi bandari inaendeshwa na muwekezaji.” Ameeleza Chris Lukosi.
Mwenyekiti Wamiliki wa Malori Tanzania, Chuki Shabani ameomba ubora wa bandari uzingatiwe ili kupata mizigo, amesema isiwe bandari peke yake ile sehemu ya maji, iangaliwe pia hiyo mizigo itafikaje inakokwenda.
“Pale inapotokea uwekezaji ambao una tija kwetu sisi ni muhimu zaidi, tungependa sana uwekezaji wa bandari utizame bandari kwa upana wake pamoja na barabara zake.” Amesema Chuki Shabani.
“Suala la bandari kwetu sisi ni la muhimu sana, kwa sababu bila mizigo hatuwezi kufanya biashara ipasavyo, ukisikia kuna nchi nane ambao ni wadau wa bandari yetu, karibu asilimia 70 au 80 wanategemea kusafirisha mizigo kupitia malori yetu.” Ameongeza.
Katibu Mtendaji, TAFFA Elitunu Mallamia amefafanua kuna haja ya uwepo wa uwekezaji wa bandari kwa sababu teknolojia ikisonga mbele na kuongeza kuwa uwekezaji unafanyika bandarini ni mkubwa.
Mdau mwingine ambaye ni Wakili kutoka Ofisi ya Mawakili ya Lux Attorney, Soba Sang’aya amesema Tanzania ni nchi kikatiba yenye utaratibu kwa mikataba ya kimataifa inaweza kuwa sehemu ya sheria au utekelezaji ndani ya nchi.