Wadau waguswa maendeleo ya afya Geita

WADAU wa Maendeleo kutoka Kampuni ya Isamilo Supplies Limited, wameeleza kuridhishwa na maendeleo ya sekta ya afya katika Manispaa ya Geita na kuamua kuiunga mkono serikali.

Meneja Mkuu wa Isamilo Supplies Limited, Robison Mageta amesema hayo kwa niaba ya kampuni wakati wa kukabidhi vifaa vya afya na michezo iliyofanyika ofisi za manispaa hiyo.

Amesema msaada huo wenye thamani ya Sh milioni 10 wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) unahusisha kitanda cha kujifungulia, magodoro, seti 70 za mashuka na mipira ya pete, kikapu na mpira wa miguu.

“Hii ni kuonyesha kwa manispaa yetu ya Geita katika kukuza sekta ya michezo na sekta ya afya. Afya ni uzima kwa hiyo unapofanya kitu kwenye sekta ya afya unatengeneza uzima kwa mtu, na michezo pia ni ajira na afya”, amesema.

Muuguzi Mkuu wa Manispaa ya Geita, Caritas Ntambi ameishukuru kampuni ya Isamilo kwa msaada wa magodoro na kitanda cha kujifungulia kwani bado kuna mahitaji hasa kwenye vituo vipya vya kutolea huduma za afya.

“Kuna vituo vya afya na zahanati ambazo zinajengwa na serikali, vifaa vilivyopo bado havijatosheleza, na kuna vituo vipya vimejengwa hivi karibuni kama sita, bado vina uhitaji wa vitanda vya kujifungulia” amesema.

Ntambi amesema mbali na msaada huo halmashauri ya manisipaa hiyo pia inaendelea kuagiza vitanda na magodoro kupitia Bohari ya Dawa (MSD) kwa ajili ya zahanati na vituo vya afya ili kukidhi mahitaji.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya mji wa Geita, Ndalo Samson ameahidi vifaa hivo vitatumika kadri ya malengo, yaliyokusudiwa kwani vituo vya kutolea huduma kwa sasa bado vina uhitaji wa vifaa mbalimbali.

“Kwa hiyo sisi tutoe wito hii isiishie tu kwa kampuni ya Isamilo, hata wengine ambao wapo kwenye jamii yetu inayozunguka Manispaa yetu ya Geita tuwakaribishe kusaidia katika maeneo mengine” amesema.

MWISHO

Habari Zifananazo

Back to top button