Wadau wataka somo la kodi liwepo shuleni

WADAU wa Maendeleo mkoani Shinyanga wameeleza suala la kodi lianze kufundishwa mashuleni ili kuondoa kero na changamoto zinazojitokeza hasa ukwepaji wa kodi kwa wafanyabiashara.

Ushauri huo umetolewa na baadhi ya wadau akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro wakati wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi ilipofika mkoani hapa kupokea maoni kero, changamoto na mapendekezo.

Mtatiro alisema walimu wapewe miongozo ya namna ya kuwafundisha wanafunzi kuanzia shule za msingi kwani itachukua muda mrefu kuwaelimisha wafanyabiashara ambao wengi hawapendi kulipa kodi wamekuwa wakikwepa.

Advertisement

“lakini wanafunzi wakipewa elimu wataanza kuzoea namna ya kulipa kodi na manufaa yake watakapo anzisha biashara zao watafahamu faida za kodi na hawatakwepa,”alisema Mtatiro.

Mtatiro alisema suala la kuchukua risiti mtu akinunua bidhaa limekuwa gumu wengi hawachukui risiti wakati mwingine wafanyabiashara wamekuwa wakiwafundisha wateja kukwepa kodi.

Mwakilishi wa vituo vya wauza Mafuta Wilaya ya Kahama Manyengo Bagedi alisema kero iliyopo ni uwepo wa utitiri wa kodi zinazo tozwa na mamlaka tofauti tofauti mapendekezo aliyotoa kodi itolewe kwa mlango mmoja ili mamlaka hizo zigawane zenyewe.

Mshauri wa masuala ya kodi mkoani Shinyanga Samweli katamba alisema risiti anazokuwa nazo mfanyabiashara imekuwa ni changamoto wakati wa ukaguzi kutofanana na ofisi ya Mamlaka ya Mapato (TRA) jambo ambalo limekuwa likiwatesa wafanyabiadhara.

Mwakilishi wa Tume ya Rais ya Mapendekezo ya Kodi Leonard Mususa kwa niaba ya mwenyekiti wa tume hiyo Ombeni Sifue alisema tume iliundwa  Oktoba 4, 2024 ikiwa na wajumbe tisa na imekwisha zunguka baadhi ya mikoa wamechukua,kero, Maoni na Mapendekezo na yatachakatwa na kufanyiwa kazi.

“Kuundwa kwa tume hii Rais anataka kuondoa kero kwa wafanyabiadhara ili kila mmoja apate haki ya msingi na Halmashauri zinatakiwa zitoe mapendekezo sio yaliyozungumzwa na wadau wengine yanatosha”alisema Mususa.