Wafanyabiashara Ghorofa K’koo wadai fidia Sh Bil.40

DAR ES SALAAM; WAFANYABIASHARA 50 waliokuwa wamepanga fremu katika jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo, Novemba 16, 2024, wamefungua kesi Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi wakidai fidia ya Sh bilioni 40 dhidi ya wamiliki wa jengo hilo.
Fidia hiyo inadaiwa kutokana na uzembe wa ujenzi wa chini kwa chini uliofanyika kinyume na makubaliano na hatimaye kusababisha kuporomoka kwa jengo hilo na kusababisha biashara zao za rejareja na jumla kuharibiwa.
Katika hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani na wakili Peter Madeleka, imeelezwa kuwa walalamikaji, wakiongozwa na Kanali Naftal Swai na wenzake 49, walikuwa wakifanya biashara katika jengo lililoko kiwanja namba 12, kitalu namba 7, eneo la Kariakoo, Manispaa ya Ilala mkoani Dar es Salaam.
Walalaikaji wanaiomba mahakama itamke kuwa walalamikiwa Zenabu Ismail (mwakilishi kisheria wa marehemu Abdallah Salim), Ashour Ashour (mwakilishi wa marehemu Awadhi Ashur Abeid) na Leondela Mdete walikiuka mkataba wa upangaji kwa kufanya ujenzi wa kizembe bila idhini.
Katika madai yao, walalamikaji wanadai kuwa kati ya Januari 2023 hadi Desemba 31, 2024, waliingia mikataba ya upangaji kwa mdomo na maandishi na walalamikiwa na kwamba waliwekeza katika biashara mbalimbali, huku thamani ya jumla ya uwekezaji na mali zilizoharibika ikikadiriwa kuwa Sh bilioni 40.
Wamedai walalamikiwa walikiuka masharti ya upangaji kwa kufanya ujenzi usioidhinishwa na usio salama, hali iliyochangia jengo hilo kuporomoka na kuwasababishia hasara kubwa.
Kutokana na hali hiyo, wanaiomba Mahakama itoe hukumu na amri dhidi ya walalamikiwa pamoja na kuwalipa gharama za uendeshaji wa kesi.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Mohamed Gwae na ilitajwa jana mbele ya Naibu Msajili Rose Kangwa.