Wafanyabiashara kortini hasara ya bil 6/- TRA

WAFANYABIASHARA watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka matano likiwemo la kukwepa kodi na kusababisha hasara ya Sh bilioni 6.2.

Wafanyabiashara hao ni Sibtain Murji, Zameen Murji na Arafat Nasir. Sibtain na wenzake wamesomewa mashitaka na wakili wa serikali, Sylivia Mitanto, Auntie Chilamula mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ferdinadri Kiwonde.

Akisoma hati ya mashtaka, Mitanto alidai kuwa kati ya Januari 2021 na Desemba 2022 jijini Dar es Salaam washtakiwa Sibtain na Zameen Murji walishindwa kuwasilisha tamko la mapato la biashara iliyosajiliwa kwa jina la Murji Brothers na hivyo kukwepa kodi ya Sh bilioni 6.2.

Katika shitaka la pili alidai kati ya mwaka 2021 na 2022 jijini Dar es Salaam, washitakiwa Zameen na Nasir walishindwa kupeleka tamko la mapato la biashara iliyosajiliwa kwa jina la Zain Slim Cut Butcher na kukwepa kodi ya Sh bilioni 1.6.

Katika shtaka la tatu, inadaiwa kuwa kati ya 2021 na 2022, Sibtain na Zameen kwa makusudi walikwepa kulipa kodi na kuisababishia (TRA) hasara ya Sh bilioni 6.2.

Katika shtaka la nne, inadaiwa kuwa washitakiwa namba mbili, Zameen na namba tatu, Arafat kwa pamoja na kwa makusudi, walikwepa kulipa kodi na kuisababishia (TRA) hasara ya Sh bilioni 1.6.

Mitanto alidai kuwa katika shitaka la tano la utakatishaji fedha, Sibtain na Zameen walijipatia kiasi cha Sh bilioni 6.2 wakati wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu wa kukwepa kodi, Mitanto alidai upelelezi haujakamilika na kuiomba mahakama tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button