Wafanyabiashara Soko la Kariakoo waandamana

DAR ES SALAAM; Wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wameandamana mpaka Ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Lumumba jijini Dar es Salaam, wakidai wanataka kujua mustakabali wao baada ya majina yao kukosekana kwenye orodha iliyotolewa na Shirika la Masoko ya Kariakoo.

Wafanyabiashara hao ambao walitakiwa kufika viwanja vya Mnazi Mmoja leo asubuhi kuwasilisha malalamiko yao, wamesema hawawezi kuendelea kuwasiliana na waratibu wa jambo hilo, kwani wamekuwa wakiorodhesha majina kila mara na matokeo yake wamekatwa na kurejeshwa majina 891 kati ua 1662.

SOMA:https://habarileo.co.tz/wafanyabiashara-891-kurejeshwa-sokoni-kariakoo/

“Sisi tunataka wafanyabiashara wote turudi Kariakoo kama alivyotuahidi Rais Samia Suluhu Hassan, na wote tunajuana, majina yaliyotoka wengi hatuwafahamu,” amesema Ashura Mhala Mwenyekiti wa Wanawake wauza Pembejeo Sokoni Kariakoo.

Akizungumza kwa niaba ya serikali,  Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, amewaahidi wafanyabiashara hao kuwa serikali itawasikiliza na kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake.

“Kesho kuanzia saa 2 asubuhi wote tuonane kwa Mkuiu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Albert Chalamila),wote mtapata haki yenu,” amesema.

Soko la Kariakoo linatarajiwa kuanza upya baada ya kuungua na kuteketeza mali za wafanyabiashara Julai mwaka 2021. Serikali imetoa Sh bilioni 28 kwa ajili ya ukarabati na kujenga soko jipya.

 

Habari Zifananazo

Back to top button