Wafanyakazi MOI wafundwa utoaji huduma za afya

WAFANYAKAZI wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wametakiwa kuwatanguliza wananchi mbele kwa kuwapa huduma nzuri badala ya kutanguliza maslahi ya kifedha zaidi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika kikao cha Nne cha baraza la wafanyakazi wa MOI Mwenyekiti wa baraza hilo na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Prof Abel Makubi aliwasisitiza kutoa taarifa sahihi na wasiwe kikwazo cha kuwakwamishaa wananchi kupata huduma kwa haraka.

Advertisement

“Moja wapo kitu ambacho wananchi wanasifia ni huduma kwa wateja na lugha nzuri ingawa kuna changamoto ya kuchelewa kupata baadhi ya huduma na hili ni suala ambalo hatuwezi kumaliza haraka kwani sio suala la mtu mmoja na tunaendelea kufanyia kazi kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa muda mfupi bila kuzungushwa,”ameeleza.

Aidha Prof Makubi ameshauri kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa ulipaji posho za ziada kwa watumishi kwa kutumia kigezo cha matokeo za ziada baada ya kufikia lengo badala ya mfumo wa sasa wa muda wa ziada (extra duty) ili kuongeza ufanisi kazini.

Amesema ni vema kuangalia upya kigezo hicho ili kuongeza ufanisi na tija kazini.

“Tuhame kutoka kwenye mfumo wa kulipana muda wa ziada (extra duty) hadi kufikia utendaji wa ziada (extra performance), hatuwezi kuendesha taasisi kwa mfumo wa ‘extra duty’, unatakiwa ulipwe kwa utendaji wa ziada, kwahiyo tuende kwa mfumo huo wa ‘extra performance.

Amefafanua kuwa mtumishi anaweza kuja kazini saa 12 asubuhi hadi saa mbili usiku na kulipwa muda wa ziada, lakini watakuja kuangalia ndani ya muda huo amefanya nini?.

“Tunataka mtu afanye kazi ya ziada ili alipwe ni sawa lakini pia tuangalie ndani ya muda huo amehudumia wagonjwa wangapi ?

Amewataka watumishi kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma bora kwanza na kuhakikisha bidhaa za huduma zipo , na ndipo pia motisha zitaendelee kuboreshwa.

“Kikao kitatuwezesha kutujulisha wapi tulikotoka na wapi tulipo na tunakokwenda, kikubwa kutatua changamoto ili kuboresha huduma, wananchi wanatutegemea na eneo kubwa wanaolotegemea wananchi ni utoaji wa huduma”