GEITA – Wafanyakazi wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) nchini Tanzania wameendelea na mgomo wa chakula kwa siku ya pili kushinikiza uongozi wa kampuni hiyo kutimiza ahadi yake kuhusu gharama za elimu ya watoto wao.
Wafanyakazi hao ambao idadi yao bado haijafahamika wamesusia chakula wakiitaka GGML kuendelea kutekeleza ‘Mkataba wa Hali Bora’ ambao pamoja na mambo mengine umeweka utaratibu wa mwajiri kusaidia wafanyakazi.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Mwajiri atawajibika kutoa msaada wa elimu kwa watoto wa wafanyakazi wake wanne wenye umri kati ya miaka 3 hadi 22 (ikiwa wako shule/chuo) kwa malipo ya Sh milioni 2.5 kwa kila mmoja mwanzoni mwa mwaka.
Kwa maana hiyo mfanyakazi mwenye watoto wanne hupokea kiasi cha Sh milioni 10 kabla ya kodi. Katika mahojiano na mwandishi wa habari hii, wafanyakazi hao ambao majina yao yanahifadhiwa wameiambia HabariLEO kuwa mpango huo uliingia matatani mwaka huu baada ya mwajiri kushusha kiwango hicho kutoka Sh milioni 10 hadi Sh milioni 7.5.
“Mwajiri alianza kupendekeza kuwa anataka kila mfanyakazi apewe malipo hayo hata kama hana mtoto … hili ni sawa. Kibaya ni kwamba alitaka ili wazo lake lifanikiwe kila mfanyakazi atapokea Sh milioni 2.5 hii haikuwa sawa na baada ya mvutano alikubali kuongeza hadi Sh milioni 7.5,” alisema mfanyakazi huyo.
“Wote tumesusia chakula. Hatutaki kwa kuwa tuna watoto wako shule, wale ambao hawana watoto wanaona kiasi hicho ni sawa, lakini si sawa,” aliongeza.
Mfanyakazi mwingine ambaye jina lake pia tunalihifadhi alisema wao wanaadhibiwa kwa makosa ya wachache kwa kuwa inaonekana kuna watu waligushi vyeti vya watoto ili wajinufaishe na utaratibu huu. “Nadhani Mwajiri alipaswa kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria juu yao lakini sio kuwaadhibu wote,” alisema.
Wafanyakazi hao wanadai maamuzi ya GGML kupunguza posho ya elimu hayana msingi wakidai kuwa mgodi huo mkubwa wa dhahabu ulitengeneza faida ya zaidi ya Sh trilioni 5 mwaka 2023. Ikiwa mpango wa GGM utafanikiwa maana yake watakata posho hiyo kwa karibu Sh bilioni 2 kutoka Sh bilioni 18 hadi Sh bilioni 16, taarifa ya wafanyakazi hao ilidai.
HabariLEO iliutafuta uongozi wa GGML ili kutoa ufafanuzi bila mafanikio.
Saa tano baadaye, taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Duran Archery ilisambazwa mgodini hapo kutoa ufafanuzi juu ya mgogoro huo.
Katika taarifa hiyo, Archery anasema taarifa ya pamoja iliyotolewa Novemba 29 kuhusu posho ya elimu haikueleweka ilivyokusudiwa na pengine kuna upotoshaji uliosababisha wafanyakazi kususia chakula cha mamilioni ya shilingi.
“Naomba kutoa ufafanuzi kuwa neno ‘until further notice’ katika taarifa ya pomoja kuhusu posho ya chakula haimaanishi majadiliano yamesitishwa. Pande zote zilitumia neno hilo kutoa nafasi kutafakari maeneo mengine baada ya kurejea kutoka Mwanza. Bado tuna muda kabla ya siku ya mwisho ya malipo abayo ni wiki ya kwanza ya Januari 2025,” ameandika kupitia taarifa ya kawaida ya Kampuni ambayo HabariLEO imeiona.
Wakati wafanyakazi wamesisitiza hawatakula kutaka kampuni hiyo iondoe gharama za chakula hicho na kuweka kwenye posho ya elimu, GGML imewaomba waendelee na ratiba zao za kawaida za chakula.
Imesema nia hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.