WASHINGTON: IKIWA ni wiki chache baada ya ajali ya ndege mbili kutokea karibu na uwanja wa ndege wa Reagan mjini Washington DC, Utawala wa Rais Donald Trump umeanza kufuta kazi mamia ya idara ya safari za anga.
Mkuu wa Shirikisho la Usalama wa Safari za Ndege (FAA), David Spero, amesema wafanyakazi waliokuwa wameajiriwa hivi karibuni walikuwa wa kwanza kupokea barua pepe iliyowaeleza kuwa wamefutwa kazi.
Miongoni mwa wafanyakazi walioathiriwa ni pamoja na wasimamizi wa mitambo na wasimamizi wa kuruka na kupaa kwa ndege, kwa mujibu wa taarifa ya mmoja wa wafanyakazi ambaye hakutaka kutajwa jina lake kutokana na kutokuweza kuzungumza na vyombo vya habari.
Shirikisho la Waratibu wa Safari za Ndege (FAA), lilisema kuwa linafanya tathmini ya athari za usalama wa safari za ndege kufuatia hatua hii ya kufutwa kwa wafanyakazi.
Taarifa zilisema kuwa wafanyakazi hao wanafutwa kazi wakati tayari kulikuwapo na upungufu wa wafanyakazi katika idara hiyo.