WATOTO wawili ambao ni wa familia moja wamekufa baada ya kutumbukia kwenye shimo la choo linalojengwa.
Akizungumza na vyombo vya habari mkoani Tabora, Kamanda wa Polisi, Richard Abwao alisema tukio hilo lilitokea Aprili 4, mwaka huu saa 10 jioni katika kijiji na kata ya Itetemia, Manispaa ya Tabora.
Aliwataja watoto waliokufa ni Rashid Hamis (3) na Sada Juma (mwaka mmoja na nusu) wote wa familia moja ambao walikuwa wakicheza maeneo ya shimo hilo.
Kamanda huyo wa polisi alisema watoto hao walifariki kutokana na kunywa maji mengi katika shimo hilo lililojaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Wiki chache zilizopita katika Kata ya Mtendeni, Manispaa ya Tabora watoto wawili pia wa familia moja walikufa maji wakati wakicheza katika dimbwi la maji.
Dimbwi hilo lililopo eneo la Kidatu limetokana na uchimbaji wa udongo kwa ajili ya ujenzi wa barabara.