WATU wasiojulikana wamefukua kaburi na kuondoa sehemu za siri za mwili wa marehemu Ruben Kasala (74) uliozikwa saa 11:30 jioni Machi 18, 2023 Kijiji cha Kasokola, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Akizungumza mtoto wa marehemu Kasala, Frank Kasala, amesema baba yao alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya sukari na pia alikuwa na shida kwenye mapafu, alifariki Machi 18, 2023 asubuhi na siku hiyo hiyo jioni wakazika.
“Kama ilivyo taratibu mnapozika, asubuhi siku inayofuata lazima wanafamilia mrudi makaburini, baada ya kurudi tukakuta kaburi limechimbwa na mwili wa baba yetu umefukuliwa, sanduku limevunjwa kabisa, wakavuta sanduku wakatoa kisha wakarudisha wakafukia kidogo na udongo, hatujajua nini kilichofanyika tunasubiri uchunguzi wa serikali ili kujua kilichofanyika,” amesema Frank Kasala.
Baadhi ya ndugu wengine wa marehemu wamesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizo na kusema kuwa mpaka sasa hawajatambua sababu kubwa iliyosababisha mwili huo kufukuliwa, huku wakihusisha tukio hilo na imani za kishirikina.
Naye shuhuda wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Hamis, amesema walipofika eneo la tukio walikuta sanduku likiwa linaonekana na baadhi ya viungo kama mguu vilikuwa vikionekana nje ya sanduku.
“Tukio hili limezua taharuki kubwa ndani ya Kata ya Kasokola kwa kuwa ni kitu ambacho hakikuwahi kutokea, mpaka sasa hatujui tunafanyaje, binadamu tumekosa hofu ya mungu hii ni kama laana, kuna watu hawatambui uwepo wa Mungu,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kasokola, Carlos Joakim amesema alipokea taarifa ya kifo majira ya saa 1:30 asubuhi, walikubaliana kuzika siku hiyo hiyo, lakini siku iliyofuata alipata taarifa ya kuwa kaburi hilo limefukuliwa na kuamua kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi.
“Tukio hili limetusikitisha na kutia aibu kijiji, Serikali ina mkono mrefu ichunguze kwa kina na waliofanya tukio hili wakamatwe na sheria ifuate mkondo wake, ili tukio hili lisijirudie tena,” amesema.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Alli Hamad Makame amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akihusisha tukio hilo na imani za kishirikina.
“Tulipofunua ile coffin (Jeneza) ikabainika kwamba sehemu za siri za huyo marehemu zilikuwa zimeondolewa, na baadae kurudisha mfuniko ule wa coffin, wakarudishia na udongo,” amesema.
Kamanda Makame amewaasa wananchi wa Mkoa wa Katavi kuachana na imani potofu zinazopelekea hadi kwenda kufukua miili ya marehemu ambayo tayari imeshasitiriwa kwa mujibu wa taratibu za dini.
“Yeyote tutakayembaini tutamkamata na kumfikisha mahakamani, sisi tunaendelea na uchunguzi na yeyote tutakayembaini kuhusika na tukio hilo tutamchukulia hatua,” alisema.
Baada ya Jeshi la Polisi kujiridhisha na uchunguzi wameamuru mwili wa marehemu kuzikwa tena.