Wafundishwa mbinu mpya utoaji uvimbe kwenye ubongo

Wafundishwa mbinu mpya utoaji uvimbe kwenye ubongo

MADAKTARI bingwa wa ubongo na uti wa mgongo wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili(MOI) jijini Dar es Salaam, leo wameanza kufundishwa mbinu mpya na ya kisasa ya kutoa uvimbe katika ubongo na uti wa mgongo, ili kuongeza ujuzi wa namna rahisi ya kuwahudumia wagonjwa wenye uvimbe kwenye ubongo.

Akizungumza katika kongamano la kimataifa la siku tano la madaktari bingwa wa ubongo ambalo limejikita katika matibabu ya uvimbe, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respisious Boniface, amesema kongamano hilo litaenda kwa vitendo zaidi na masomo ya darasani,  ambapo watu watano hadi 10 watapatiwa huduma.

 

Advertisement

“Leo tunaanza kongamano la siku tano lililoratibiwa na MOI  na Chuo Kikuu cha Colorado nchini Marekani hili ni la pili, kwanza ilikuwa 2019, hili limejikita katika matatizo ya uvimbe ambao unatokea  katika ubongo na uti wa mgongo, tuko hapa kufundisha mbinu mpya za kutibu, kwani kila siku inaibuka mbinu mpya wenzetu wakiendelea wanatuletea na sisi tutumie mbinu hizo kulingana na dunia,” amesema.

Amesema kila siku kunaibuka mbinu mpya kama upasuaji  unatumia siku moja, inaletwa mbinu nyingine ambayo upasuaji unachukua muda mfupi zaidi ya hapo, hivyo mbinu ya mwaka 2019  inakuwa inakuwa ya zamani.

Amebainisha kuwa baada ya kongamano hilo, wanatarajia kuwa  mbinu za kutibu wagonjwa zitakuwa zimeimarika zaidi na salama zaidi.