Waganga wafawidhi kupewa posho

SERIKALI imepanga kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 kuwalipa waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi nchini posho za madaraka kutokana na kazi kubwa wanayofanya.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa taarifa hiyo leo Februari 14, 2024 akifunga mkutano wa mwaka wa waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi uliofanyika jijini Dodoma.

“Waganga wafawidhi mnastahili kulipwa posho ya madaraka, mnafanya kazi kubwa kwenye vituo vya kutolea huduma ninyi ndio madaktari, wafamasia, wataalam wa maabara, mnasimamia ujenzi wa miradi ya Serikali hakika mnastahili kulipwa posho hii”.

Advertisement

amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watumishi wanakuwa na mazingira wezeshi ya kufanya kazi pamoja na motisha kazini hivyo Serikali pamoja na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohammed Mchengerwa watahakikisha wanaenda simamia suala hilo ili waganga wafawidhi wa vituo waanze kupata posho za madaraka.

Ummy amewataka waganga wafawidhi kuhakikisha wanaendela kusimamia ubora wa huduma za afya katika vituo wanavyovisimamia, kusimamia vyema miradi ya maendeleo inayofanyika katika vituo vyao na kuhakikisha watumishi walio chini yao wanafanya kazi kwa ufanisi ili kutimiza azma ya Serikali ya utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.