ETHIOPIA : WAGOMBEA wa Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika wanatarajiwa kukabiliana leo ana kwa ana katika mdahalo wa kuonyesha uwezo wao wa kazi.
Mdahalo huo kuhusu Afrika utafanyika katika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa.
Miongoni mwa wanaoshiriki ni mgombea wa Kenya katika nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Raila Odinga.
Wagombea wengine wanaoshiriki mdahalo huo ni Waziri wa mambo ya nje wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascr Richard Randriamandrato.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritius Anil Kumarsingh Gayan, alijiondoa mapema katika mchakato huo.
AU imesema mdahalo huo wa Afrika ni jukwaa muhimu kwa wagombea kuhutubia raia wa Afrika katika mdahalo wa televisheni, unaorushwa moja kwa moja.
Wagombea watawasilisha maono na mawazo yao juu ya utekelezaji wa Ajenda 2063 ya AU. SOMA: Odinga kugombea uenyekiti wa Tume AU
“Mjadala unaangazia masuala ya sera na ushiriki wenye mwelekeo wa suluhu kuhusu jinsi kila mgombea anavyopanga kuendeleza utimilifu wa matarajio na malengo ya ajenda ya 2063, miradi mingine ya AU yenye mwelekeo wa bara, na misimamo ya pamoja ya Afrika,” AUC inasema.