MKUU wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amewaomba wagombea wote ambao hawajaridhishwa na uteuzi kufuata taratibu zilizopo kwa ajili ya kuwasilisha pingamizi.
Sawala ametoa ombi hilo leo Novemba 10, 2024 kwa wagombea wote walioteuliwa na vyama vyao vya siasa na kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika halmashauri zote tisa za mkoa wa Mtwara unaotarajiwa kufanyika Novemba 11,2024.
Amesema endapo mgombea yoyote hakuridhika na uwamuzi uliotolewa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi au anapinga uteuzi wa mgombea yeyote anaweza kuwasilisha pingamizi kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi ambae atalishughulikia pingamizi hilo ndani ya siku mbili.
Ameongeza kuwa kama mgombea hatoridhika na uwamuzi wa msimamizi msaidizi atakuwa na haki ya kukata rufaa kwenye kamati ya rufaa.
“Niwaombe wagombea wote ambao kwa namna moja ama nyingine hawakuridhika na uteuzi kufuata taratibu zilizopo kwa kuwasilisha pingamizi ili shughuli hizi za uchaguzi ziendelee kwa amani na utulivu katika mkoa wetu wa Mtwara.”amesema Sawala
Hata hivyo amewapongeza na kuwataka viongozi wenye dhamana ya kusimamia na kuratibu mchakato mzima wa uchaguzi kuendelea kuratibu zoezi hilo la uchaguzi kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu zilizopo na kusimamia haki kwa vyama vyote na kuwapa fursa ya kupokea mapingamizi ambayo waliyapokea.
Sambamba na hilo amewaomba vyama vya siasa kuendelea kudumisha amani katika kipindi ambacho mchakato wa Uchaguzi unaendelea na kutoa rai kwa watendaji wote ikiwemo wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na wasimamizi wakuu kuhakikisha wanaendelea kufuata kanuni na muongozo wa uchaguzi katika kutekeleza na kusimamia mazoezi yote ya uchaguzi yanayoendelea.