DAR ES SALAAM: JUMLA ya wagonjwa 40 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha nyonga katika kambi maalum ya matibabu iliyoanza Februari 26 hadi Machi 1,2024 katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Kambi hiyo itafanywa na madaktari bingwa wa MOI na madaktari bingwa kutoka nchini Pakistan.
Akizungumzia kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Prof. Abel Makubi amesema amewapokea madaktari bingwa wabobezi wa upasuaji wa nyonga Watatu kutoka nchi ya Pakistan.
Kambi hiyo pia itatumika kama sehemu ya kuwajengea uwezo wa umahiri madaktari wazawa.
“Nashukuru kwa kuja kwenu, mjisikie mko nyumbani na iwapo mtapata changamoto yeyote msisite kuwasiliana nasi, uwepo wenu hapa ni wa umuhimu kwetu, tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu muhimu kwa ustawi wa maendeleo ya tiba hapa MOI” amesema Prof. Makubi
Kwa upande wake kiongozi wa wataalam hao kutoka Pakistan, Abdullah Amjad ameushukuru uongozi wa MOI kwa mapokezi mazuri, ukarimu na ushirikiano walioupata.
“Tunashukuru kwa mapokezi mazuri, na tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu mzuri” amesema Amjad
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Mifupa, Nyonga na Magoti Dk. Athony Assey amesema kambi hiyo imeanza kwa upasuaji wa wagongwa wawili na baadae kuendelea na wengine hadi Machi, 01, 2024 kambi hiyo itakapomalizika.