Wagonjwa 9,545 wafanyiwa upasuaji mabusha
MKURUNGENZI Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk William Kisinza amesema takribani wagonjwa 9,545 nchini wamefanyiwa upasuaji wa mabusha.
Amesema wagonjwa 3,115 kati yao ni kutoka mkoa Lindi na kwamba upasuaji huo ulifanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wengine nchini.
Dk Kisinza amesema hayo leo, mkoani Lindi katika Kongamano la uwasilishaji wa matokeo ya utafiti wa ugonjwa wa mabusha na matende uliofanywa na NIMR kupitia mradi wa Kupambana na vikwazo vya kutokomeza matende na mabusha nchini.
Amesema Kati ya mwaka 1998 na 2004, NIMR ilifanya utafiti nchini, ambapo Mkoa wa Lindi ulibainika kuwa na kiwango cha maambukizi ya matende na mabusha kati ya asilimia 47 na 60 katika Halmashauri za Nachingwea, Liwale na Mtama.
“Utafiti huo ulipelekea kuanzishwa kwa Mpango wa Taifa wa kutokomeza ugonjwa wa matende kwa kutumia afua ya ugawaji wa dawa za kingatiba za ‘Albendanzole na Ivermectin’ katika ngazi ya jamii,” amesema.
Amesema kutokana na juhudi hizo, maambukizi ya magonjwa hayo yamepungua na kufikia kiwango cha kati ya asilimia 2.
3 na 6.2 katika Halmashauri za Nachingwea, Liwale na Ruangwa mkoani.