WAGONJWA katika Hospitali ya Isaka iliyopo Halmashauri ya Msalala Mkoa wa Shinyanga watanufaika na vitanda 50 vyenye magodoro pamoja na shuka 200 msaada ulitolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA)
Meneja Uhusiano na Mawasiliano TPA, Nicodemus Mushi amesema msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh million 68.9 ni sehemu ya utaratibu wa mamlaka kurudisha faida kwa jamii.
“Hii sio mara ya kwanza kufanya kitu kama hiki kwa jamii inayozunguka bandari yetu kavu hii ya Isaka. Mwaka jana tulitoa mabati 315 kwa ajili ya jengo la wodi ya mama na mtoto.” alisema.
Mganga mfawidhi wa kituo hicho, Immaculate Matete amesema msaada huo umekuja wakati muhimu kwani kulikua na changamoto ya uhaba wa vifaa hivyo.
“Tulikuwa na vitanda na godoro 60. Sasa idadi imefikia 110 tunashukuru kwa msaada,’ alisema.
Diwani wa kata ya Pazi Majuto alitoa shukrani kwa msaada endelevu wa TPA, akwaomba wadau wengine kuunga mkono juhudi hizo kwani bado kituo kina mahitaji mengi ya muhimu ikiwemo jokofu la kuhifadhia maiti.
Amesema wananchi wanalazimika kusafiri umbali mrefu kupeleka maiti Hospitali ya Wilaya Kahama, hali ambayo ni usumbufu na kuingia gharama.