Wagonjwa wa kuchuja damu waongezeka Mloganzila

Ni baada ya huduma kuboreshwa, wenye uhitajibupandikizaji figo waitwa

IDADI ya wagonjwa wanaofanyiwa huduma za kuchuja damu katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila imeongezeka kutoka wagonjwa 91 kwa kipindi cha Januari-Machi 2022 na kufikia wagonjwa 157 kwa kipindi kama hicho mwaka 2023 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 72.

Hatua hiyo inatokana na maboresho makubwa yaliyofanywa katika sekta ya afya na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza vifaa tiba na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH-Mloganzila Dkt. Immaculate Goima amesema uelewa wa dalili za magonjwa yasiyo ya kuambukiza miongoni mwa jamii umeongezeka jambo ambalo limepelekea wagonjwa kufika hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na kuanza matibabu mapema.
Dkt. Goima ameongeza kuwa Mloganzila imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii ya namna ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na pale wanapohisi kuwa na dalili za magonjwa hayo wanashauriwa kufika hospitalini mapema kwa ajili ya ushauri na matibabu badala ya mgonjwa kusubiri hatua za mwisho ndio anakwenda hospitalini.
“Mloganzila tuna wataalamu wenye ujuzi na weledi katika matibabu ya magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya figo, tunatoa huduma kwa saa 24 siku kila siku, watoa huduma wetu wana ari, morali na wanajali wagonjwa pia wanatoa huduma muda wote” amefafanua Dkt.

Goima.

Akizungumzia kuhusu huduma za kupandikiza figo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH-Mloganzila Gyunda Anthony ameeleza kuwa, Mloganzila ilifanya upandikizaji kwa wagonjwa watatu ambapo kumekuwa na mafanikio makubwa kwani wagonjwa hao na ndugu waliowachangia figo wanaendelea vizuri na kufanya shughuli zao kama kawaida.
“Wagonjwa hawa tuliowapandikiza figo Aprili mwaka huu , wanakuja kliniki kwa ufuatiliaji wa afya zao mara moja kwa mwezi , kabla ya kupandikizwa figo walikua wanafanya dialysis mara tatu kwa wiki na kukaa zaidi ya saa nne kwenye mashine ya kuchuja damu kila walipohudhuria hospitali kwa ajili ya huduma hiyo. “ amefafanua Dkt. Gyunda.
“Napenda kuieleza jamii kwamba upandikizaji wa figo ni salama kwa mgonjwa na kwa mchangia figo hivyo wale wenye changamoto za figo wanaweza kufika hospitalini hapa kupata huduma.
“Huduma hii ni endelevu na tunaendelea nayo kwa kushirikiana na wataalamu wabobezi kutoka Korea Kusini chini ya  Taasisi ya KOFIH’.

’ Amesema

Aidha, ametaja sifa za mgonjwa anayestahili kupandikizwa figo kuwa ni yule mwenye tatizo sugu la figo, umri chini ya miaka 60, asiwe na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na homa ya ini, awe na akili timamu na uwezo wa kupata dawa za kushusha kinga baada ya upandikizaji.
Ameongeza kuwa sifa za mchangia figo, awe na umri kati ya miaka 25 hadi 60, awe na afya njema ya akili, asiwe na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na homa ya ini, asiwe na ugonjwa wa kisukari wala shinikizo la juu la damu.

Dkt. Gyunda ameishauri jamii kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo kufanya mazoezi, kuzingatia ulaji sahihi kwa kupunguza matumizi ya vyakula vya wanga na sukari na pia kula matunda na mboga mboga kwa wingi ili kuepuka kupata magonjwa yasiyoambukiza.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button