Waingizaji dawa za kulevya wazidi kubanwa

BUNGE limefanya marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kuongeza idadi ya dawa zinazozuiwa kuingia nchini.

Hayo yamebainika bungeni jijini hapa jana wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dk Eliezer Feleshi akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 wa Mwaka 2022.

Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 ni moja ya sheria tatu zilizopendekezwa kurekebishwa kupitia muswada huo uliowasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza Juni 23, mwaka huu.

Advertisement

Katika marekebisho hayo zimejumuishwa kemikali bashirifu au mchanganyiko wake katika orodha ya dawa zilizokatazwa kuingizwa nchini bila kibali chini ya sheria hiyo.

Dk Feleshi alisema madhumuni ya marekebisho hayo ni kudhibiti dawa ambazo matumizi yake yanaweza kuchepushwa na hatimaye kutengeneza dawa za kulevya ambayo yanakatazwa na sheria hiyo.

Kwa mujibu wa muswada huo, marekebisho pia yanawapa maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) nguvu za kisheria sawa na mamlaka waliyonayo maofisa wa polisi chini ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 au mamlaka waliyonayo maofisa forodha chini ya Sheria ya Usimamizi wa Ushuru wa Forodha Sura 403.

Dk Feleshi alibainisha kuwa marekebisho yaliyopendekezwa ofisa wa mamlaka anaweza kuwasiliana na kushirikiana na mamlaka nyingine pale panapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo na lengo ni kuboresha utendaji wa maofisa wa mamlaka kwa kuwapa mamlaka toshelezi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Marekebisho hayo pia yamehusisha kumpatia mamlaka mkurugenzi mkuu au ofisa aliyeidhinishwa na mamlaka uwezo wa kutoa hati za upekuzi na lengo la marekebisho hayo ni kuiwezesha mamlaka kutekeleza majukumu yake kiupelelezi kwa ufanisi zaidi hususani pale mamlaka inapotakiwa kuchukua hatua za haraka ili kuzuia kuharibu au kutorosha ushahidi.

Awali Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, ilisema nchi iko katika vita kali ya mtandao wa biashara ya dawa za kulevya hivyo mapendekezo yaliyotolewa ni muhimu katika kuchochea juhudi za serikali kudhibiti biashara hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Najma Murtaza Giga amesisitiza mamlaka kuendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vingine ili kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya biashara hiyo.

Akijibu hoja baada ya kuwasilisha muswada huo, Dk Feleshi alisema lengo la marekebisho na kutunga sheria hizo ni kuwezesha mamlaka husika kufanya kazi zake vizuri na ni ushahidi tosha serikali ilihitaji yafanyike marekebisho ya sheria na kukidhi mahitaji husika.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema lengo la sheria hiyo ni kuhakikisha mamlaka husika inafanya kazi kwa umakini na ufanisi na kudhibiti tatizo la dawa za kulevya.