Waiomba serikali ukarabati wa barabara Serengeti

WADAU wa Utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti wameiomba Serikali kuwapatia suluhisho la kudumu la ujenzi wa barabara katika Hifadhi za Taifa hususani barabara ya Serengeti.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Wolway Trekking Tanzania Limited, John Macha alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA) katika kuboresha barabara hizo ambazo kwa kiasi kikubwa ziliathiriwa mvua na wingi wa magari ya utalii yanayopita kwa siku.

Macha amezungumza hayo mbele ya Kamishna ya Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Nassoro Juma Kuji, ambaye alifanya ziara ya kukagua matengenezo yanayoendelea kufanyika katika  barabara ya Naabi hadi Seronera.

SOMA: Tanzania yaingia 10 bora mapato ya utalii

Kutokana na hali hiyo wadau hao wamependekeza kujengwa kwa barabara yenye tabaka gumu katika hifadhi hiyo ikiwa ni suluhisho tatizo la barabara.

“Niipongeze Serikali kwa matengenezo haya ya barabara kutoka Seronera mpaka Golini tunafahamu hii ni kazi kubwa mnaifanya na tunaomba muendelee nayo lakini kwa ufumbuzi wa kudumu kuwe na jawabu la kudumu kwa sababu magari ni mengi mtakuwa mnafanya zoezi hili ndani ya wiki mbili mpaka tatu mnarudia zoezi hili.

“Kwa hiyo lile wazo Serikali kupitia Serengeti la kuwa na  tabaka gumu la kudumu lingekuwa wazo zuri sana wakati huu tungesahau matengenezo haya ya mara kwa mara  na hata kuongeza gharama ni bora tuingie gharama kutengeneza barabara itakayokaa muda mrefu hata kama ni gharama kubwa,” alisema Macha

Januari 26, 2024 Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Nassoro Juma Kuji alifanya ziara ya kukagua miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuiagiza menejimenti ya hifadhi hiyo, kushughulikia kwa haraka maeneo korofi ya barabara ndani ya hifadhi ili watalii wafikie azma yao ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.

SOMA: Idadi ya watalii yaongezeka kwa asilimia 96

Kutokana na hali hiyo aliilekeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kurekebisha maeneo yote korofi na kuhakikisha kuwa hakuna maeneo ambayo hayatapitika licha ya uwepo wa mvua kubwa zilizonyesha pamoja na ongezeko kubwa la magari ya utalii ili kupunguza adha kwa wageni.

“Licha ya changamoto ya mvua kubwa zinazoendelea hatuwezi kusubiri ziishe tumeazimia kushughulikia kwa haraka maeneo yote korofi ikiwa ni hatua za haraka, lakini lengo kuu ni kuhakikisha barabara hizi zinakuwa na tabaka gumu, haya ni maagizo yangu kwa menejimenti kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote,” alisema Kamishna Kuji.

Habari Zifananazo

Back to top button