Waipongeza TEA kuboresha miundombinu ya elimu
WANUFAIKA wa miradi ya Mfuko wa Elimu katika Mikoa ya Arusha na Manyara, wameipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kuboresha miundombinu ya elimu, hali ambayo wamesema imechangia kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia.
Pongezi hizo zimetolewa kwa mamlaka hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye kwenye miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Elimu katika Mikoa ya Arusha na Manyara, ambapo alitembelea miradi ya ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya Sekondari Sokoni II na madarasa mengine matatu katika shule ya Msingi Kaloleni zote za jijini Arusha.
Miradi mingine iliyotembelewa katika ziara hiyo ni miradi ya ujenzi wa matundu 24 ya vyoo katika Shule ya Msingi ya Kaloleni jijini Arusha, Shule ya Msingi Gidewari pamoja na Shule ya Sekondari Dareda zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara.
Pia Mkurugenzi Mkuu wa TEA ametembelea ujenzi wa maabara ya sayansi katika Shule ya Sekondari Maganjwa ya Babati mkoani Manyara na mradi wa ufadhili wa wanafunzi wanofanya mafunzo ya utalii na ukarimu katika chuo cha VETA-Arusha yanayofadhiliwa na taasisi ya Asilia Giving kupitia Mfuko wa Elimu.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo amesema, mradi wa maabara ya sayansi katika shule ya sekondari Maganjwa katika Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Babati, utainua ufaulu wa masomo ya sayansi katika shule hiyo kwa kuwa utawezesha wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Seleman Msumi amesema, Mfuko wa Elimu umewezesha halmashauri yake kujenga madarasa matatu ya kisasa pamoja na kununua samani, ambazo ni viti na meza hali iliyosaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika vyumba vya madarasa kwenye shule hiyo.