Wajane watakiwa kuchangamkia fursa

MTWARA: WAJANE mkoani Mtwara wametakiwa kujihusisha katika fursa mbalimbali ikiwemo kilimo cha mazao mchanganyiko, uvivu na ushonaji ili waweze kujikwamua kiuchumi na kubadilisha maisha yako baada ya kuondokewa na wenza wao.
Hayo yamejiri wakati wa maadhimisho ya siku ya wajane duniani yaliyoadhimishwa kimkoa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rachel Kasanda amesema wajane hao watafute elimu ya kitu ambacho wanaweza kufanya kupitia wataalam wa maendeleo na mafunzo yanayotolewa na asasi mbalimbali za kiraia ili kubadili maisha yao.
“Fursa zipo nyingi katika mkoa wetu kwa akina mama kama mazao lishe, korosho, mbaazi, ufata na mengine ni mazao liche ambayo dunia wanayatafuta, tukifanya biashara za namna hii tunaweza kubadilisha maisha yetu”amesema Kasanda.
Pia amewata kupaza sauti zao na kuripoti matukio ya kikatili ikiwemo kunyimwa mirathi pindi wanapoondokewa na wenza wao kwa ajili ya kupatiwa haki zao kisheria.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo Athmin Mapalilo ametoa wito kwa mjane mmoja mmoja au kikundi cha wajane kuomba mkopo wa asilimia 10 unaotolewa ngazi za halmashauri kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kukuza uchumi wao.
Meneja wa Nanauka Foundation Joel Nanauka amezitaja baadhi ya changamoto zinazowakwamisha wajane kuendelea kiuchumi ikiwemo kukata tamaa ya maisha, kukaa na kuishi na maumivu ya muda mrefu bila kusamehe.
Baadhi ya wajane hao akiwemo Mary Kalisinje amekiri kupata elimu sambamba kutoa wito kwa wajane wenzao kuwa wajishughulishe na kujumuika na wengine katika kutatua changamoto za maisha.