Wajasiriamali Kigoma wanafaika mikopo ya halmashauri

WAJASIRIMALI kutoka Halmashauri ya Wilaya Kigoma ambao wamepokea mikopo kutoka halmashauri hiyo kwa ajili ya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na biashara wameishukuru serikali kwa mikopo hiyo.
Wajasiliamali hao wametoa kauli hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya Kigoma,Dk Rashid Chuachua wakati halmashauri ilipokuwa ikitoa mikopo kwa vikundi vya vijana na wanawake ambapo jumla ya vikundi 12 vimenufaika na mikopo hiyo.

Mkuu wa wilaya Kigoma Rashidi Chuachua akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi ya mkopo kwa vikundi vya wanawake na vijana ambapo jumla ya mikopo yenye jumla ya Sh milioni 209 imetolewa
Mmoja wa wajasiliamali hao, Zuhura Kassim kiongozi wa kikundi cha jipe moyo Mwandiga alisema kuwa wana kikundi cha cherehani na ufumaji hivyo mkopo huo utawawezesha kunua mota za kuendeshea cherehani za umeme, mashine za kuadirizi na baadhi yam ashine ambazo zinawezesha nguo kushonwa kwa ubora kama nguo zinazotengenezwa viwandani hivyo itawasaidia kuongeza wateja.
Naye Hungu Omari Seifu Kiongozi wa bodaboda na mabanda ya chipsi kutoka kata ya Simbo Halmashauri ya wilaya Kigoma ambao wamepata mkopo wa milioni 15 ambazo alisema kuwa watazitumia kununua pikipiki nne sambamba na kuboresha banda lao la chipsi kuwa katika mazingira ya kisasa kuifanya biashara yao kuwa na tija kubwa.

Sehemu ya wajasiliamali kutoka makundi ya vijana na wanawake waliohudhuria hafla ya utoaji mikopo kwa wanawake na vijana kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya Kigoma
Akizungumza kabla kukabidhi mikopo hiyo Mkuu wa wilaya Kigoma,Dk.Rashid Chuachua alisema kuwa baada ya mikopo hiyo kusimamishwa ili kufanyiwa maboresho kwa sasa imeanza kutolewa tena kuwezesha kusaidia makundi maakum yaweze kuimarisha shughuli zao za kiuchumi kwa namna ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan maono yake yamemuongoza katika kusaidia makundi hayo kuinua kipato chao cha kiuchumi.
Pamoja na hivyo Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa mikopo hiyo siyo sadaka wala ruzuku na inapaswa kurudishwa kwa kadri kila kikindi kilivyosaini mkataba na kuwa na andiko ambalo limewezesha mikopo hiyo kutolewa na kwamba hiyo ni hisani kubwa iliyotolewa kwa wajasiliamali hao na Rais Samia Suluhu Hassan hivyo hawapaswi kuichezea fursa hiyo.

Zuhura Kassim mjasiliamali kutoka kijiji cha Mwandiga Halmashauri ya Wilaya Kigoma ambaye kikundi chake kimenufaika na mkopo wa makundi maalum kutoka mapato ya ndani ya halmashauri.
Akitoa taarifa kuhusu utoaji wa mikopo hiyo Afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya Kigoma, Judith Allute alisema kuwa mikopo yenye thamani ya shilini milioni 209.8 imetolewa kwa wajasiliamali hao ambapo jumla ya vikundi 12 vimenufaika kati yao vikiwepo vikundi saba vya wanawake na vikundi vitano vya vijana ambapo mchakati wa kwa ajili ya vikundi vya walemavu unaendelea na Sh milioni 50 zimetengwa kwa vikundi hivyo.



