UWT yatoa cherehani kwa wajasiriamali Pemba

PEMBA: UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) umekabidhi cherehani kumi kwa wanawake wajasiriamali wanaojishughulisha na shughuli za ushonaji wa nguo katika wilaya ya Chakechake, kisiwani Pemba, ili kuwawezesha kiuchumi.

Akikabidhi cherehani hizo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, Mkoa wa Kusini Pemba, Nadra Ghulam Rashid, alisema zoezi hili ni sehemu ya sherehe za kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, na kuongeza kuwa lengo la UWT ni kuhakikisha kwamba miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanaakisi mapinduzi ya kiuchumi kwa wanawake visiwani humo.

Aidha, aliwahimiza wanawake kuanzisha miradi ya kijasiriamali ili waweze kujiimarisha kiuchumi. SOMA: Watunukiwa cherehani, mashine atamizi kujiajiri

Advertisement

Pamoja na hilo, Mjumbe huyo alikabidhi kiasi cha shilingi milioni mbili kwa ajili ya kusaidia mitaji kwa wajasiriamali katika wilaya ya Chakechake na mkoa wa Kusini Pemba, pamoja na shilingi milioni tano kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba za UWT.