IMEELEZWA wanawake wajawazito na wanaonyonyesha watapatiwa elimu ya kidigitali namna ya kufuatilia taarifa zao za afya katika vituo vya afya wanavyopatiwa huduma nchini.
Kupitia kampeni ya Taarifa ‘Yangu ya Afya’ Afya Yangu, mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Omuk Hub kutoka Kagera, Abeid Bushira alisema ni muhimu kufuatilia maendeleo yao katika vituo wanavyopatiwa huduma ili kujua mwenendo wa utunzaji wa taarifa hizo.
Akizungumza katika vituo vya afya vya Kagemu na Buhembe mapema leo Juni 12, 2023 alisema ni haki ya Mwananchi kujua taarifa hasa anaposajiliwa kwa mara ya kwanza.
Alisema lengo la shirika ni kuendelea kutoa elimu juu ya haki ya kupata taarifa za afya ili kuwawezesha wananchi kuwa karibu na afya zao, kujua hali zao za kiafya , kufuatilia hali za afya zao na kujenga tabia ya kufika katika vituo vyao ili kujua taarifa zao.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka kituo cha afya cha Buhembe, Khadija Suleiman alisema kuwa hajawai kufikiria kufatilia taarifa yake ya afya na kila mara akiumwa anaenda dukani analeta daftari jipya kwa ajili ya kujisajili kituoni hapo na kupima vipimo upya.
Aidha, amependekeza uwepo mfumo maalumu wa kielektroniki katika vituo vya afya ambao utamsajili mgonjwa na mgonjwa huyo asibebe daftari endapo akiumwa tena.
“Kwa mfano mimi nikiumwa nakuja na daftari la dukani naandikiwa majibu naenda dirishani kupata dawa alafu nalipeleka nyumbani ,nikimaliza mwaka mwingine au mtoto akaumwa naleta daftari lingine,ukiniuliza mwaka jana daftari nililotumia ni lipi siwezi kukwambia liko wapi na sijui Kama nikiuliza hapa kituoni kwamba mwaka Jana niliumwa naomba faili langu sijui Kama naweza kupata taarifa yangu kwa uharaka,nadhani Baada ya Elimu hii tunahitaji mfumo maalumu wa kusajili na kulinda taarifa zetu za Ugonjwa.”alisema Suleiman.
Mganga Mkuu Msaidizi Manispaa ya Bukoba, Lilian Kyaruzi alisema ni mara chache wananchi kuulizia taarifa zao za afya hasa wakishapata matibabu hakuna ambaye ufatilia zaidi lakini vituo vimekuwa vikitunza mafail yao ingawa nakiri kuwa yanaeeza yakawa mengi sana kwa sababu tunahudumia watu wengi.
Alisema kuwa wataalam wa afya wamekuwa wakilinda taarifa za wagonjwa huku akipongeza serikali kwa kutunga sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi ambapo alisema kuwa Huduma za afya kwa sasa zinaendelea kuimarika hivyo wananchi wategemee mabadiliko makubwa na watafikia wanapopataka hasa kusajili taarifa zao kwa mifumo ya Kielektroniki.