NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Zainab Katimba amewataka makandarasi wanaopatiwa kazi za ujenzi wa barabara za Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini( TARURA) kutekeza miradi hiyo kwa ufanisi na kwa wakati kama ilivyo makubaliano ya katana.
Katimba ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika jiji la Dar Es Saalam ya kukagua barabara za TARURA katika jiji hilo kwa majimbo ya Ukonga na Segerea na kuona maeneo zitakapojengwa barabara mpya na barabara zitakazoboreshwa katika mradi wa awamu ya pili ya uendelezaji wa Halmashauri ya jiji la Dar Es Salaam (DMDP II) katika majimbo hayo.

“Wakandarasi wanaopewa kazi hizi wanajukumu la msingi la kuhakikisha wanatimiza jukumu lao kimkataba wahakikishe barabara hizi wanazijenga kwa mujibu wa mkataba ndani ya muda kusiwe kuna kusuasua kwasababu wananchi wanataka kuona tija kubwa ambayo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria iweze kufika kwao ya kuwajengea Miundombinu mizuri ya barabara” amesema.
Katimba amesisitiza kuwa barabara hizo zinazojengwa zinasaidia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi vilevile kuwasaidia wananchi kufikia huduma za msingi za kijamii.

Kwa upande wake mbunge wa Segerea, Bonah Kamori ameiomba serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuwahimiza wakandarasi wasichelewe ili barabara hizo zijengwe na wananchi waendelee na shughuli za kiuchumi na kufikia huduma za msingi hasa katika kipindi cha mvua.

Naibu Waziri Katimba ametembelea barabara za Pugu-Majohe-Viwege kilomita 10.5, Banana-Kitunda-Kivule-Msongo kilomita 12.6 za jimbo la Ukonga na Bonyokwa-Zahanati kilimita 1.46, Bonyokwa mwisho kilomita 3.2, Segerea Kusini kata ya Segerea kilomita 0.69 za jimbo la Segerea.