Wakandarasi wanaochelewesha miradi ya maji kutolipwa

KATIKA kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa wakati serikali imesema haitatoka fedha kwa wakandarasi wanaozembea kukamilisha miradi kwa wakati.

Naibu Waziri wa maji Kundo Mathew ametoa msimamo huo akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kukagua miradi ya maji mkoani Tanga.

Amesema kuna wakandarasi wanaotekekeza miradi kwa kasi ndogo ambayo haiendani na lengo la utekelezaji wa miradi hiyo ambayo serikali imedhamiria.

“Hatutalipa fedha kwa wakandarasi ambao wameshindwa hata kupiga hatua kwenye utekelezaji wa miradi yao ni bora tuwekeze nguvu kwa wakandarasi ambao wamefikisha asilimia 70 au 80 ambao watasaidia kuongeza takwimu za upatikanaji wa maji,”amesema Naibu Waziri.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Batlida Buriani amesema licha ya jitihada kubwa inayofanywa na serikali bado wilaya za Handeni na Kilindi zina asilimia chini ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama.

Nae Meneja wa Wakala wa maji mijini na vijijini RUWASA mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo amesema mkoa huo unatekeleza jumla ya miradi 72 inayotarajiwa kukamilika mwisho mwa mwaka huu na hivyo kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 65 ya sasa hadi 85.

Habari Zifananazo

Back to top button