LICHA ya serikali kutenga miradi maalum kwa ajili ya wakandarasi wazawa katika ujenzi na maboresho ya barabara mikoani, wakandarasi wazawa mkoani Mtwara wameshindwa kujitokeza kuomba tenda hizo kwa mwaka 2022/2023 na badala yake kuchukuliwa na wakandarasi kutoka Lindi pekee.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Mtwara, Mhandisi Zuena Mvungi, amesema hayo leo wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba 18 yenye thamani ya Sh bilioni 8.165 ya ujenzi wa barabara kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
“Kwa mwaka huu wa fedha miradi minne ilitengwa kwa ajili ya makundi maalumu, kwa ajili ya wakandarasi wa Mtwara na Lindi, wakandarasi wa Mkoa wa Mtwara hawakujitokeza kuomba kazi hizo, fursa zimechukuliwa na wakandarasi wa Lindi,” amesema.
Meneja huyo ameshauri wakandarasi mkoani Mtwara, washiriki fursa za ujenzi na maboresho ya barabara za vijijini na mijini kwenye miradi maalum.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Zuena katika miradi 18 iloyosainiwa, miradi minne yenye thamani ya Sh bilioni 1.8 itatekelezwa Wilaya ya Masasi, Newala miradi mitano (Sh bilioni 2.2), Wilaya ya Mtwara miradi nane ( Sh bilioni 3.8), Tandahimba mradi mmoja (Sh milioni 231).
Amewataka wakandarasi waliosaini mikataba ya ujenzi wa miradi hiyo kuhakikisha weledi na ufanisi na kujituma zaidi kuhakikisha inatekelezwa na kukamilika kwa muda mwafaka.