Wakili aliyemtetea mjane nyama ya swala ajitosa ubunge Iringa Mjini

IRINGA: WAKILI wa kujitegemea na kada mwandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Moses Gwatengile Ambindwile, leo amechukua rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea Ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia chama hicho, akiahidi kusimama kwa ajili ya haki, maendeleo na ufanisi wa utawala bora unaozingatia sheria na utu.
Ambindwile anajulikana kitaifa kwa kuongoza jopo la mawakili waliomsaidia bila malipo mjane Maria Ngoda, aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 22 kwa kosa la kupatikana na vipande 12 vya nyama ya swala.
Hukumu hiyo ilibatilishwa na Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2023, chini ya Jaji Mugeta, na mjane huyo aliachiliwa huru — tukio lililoibua mjadala mpana wa haki za binadamu na matumizi ya sheria kwa watu wasiojiweza.
Wakili Ambindwile, ambaye pia ni Mkurugenzi na Mwanzilishi wa kampuni ya sheria ya The Icon Law Corporate Attorneys, ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kimataifa na Haki za Binadamu.

Amehudumu pia kama Msaidizi na Mshauri wa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kabla ya kujitegemea.
Kwa sasa, mbali na majukumu ya uwakili, ni Mwenyekiti wa TLS (Tanganyika Law Society) Kanda ya Iringa na Njombe, na Mshauri wa Kodi aliyeidhinishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Anahudumu kama Katibu wa Umoja wa Washauri wa Kodi mkoa wa Iringa, chombo kinacholenga kuimarisha maarifa, ushirikiano na mifumo bora ya kodi kwa maendeleo ya taifa.
SOMA ZAIDI
Katika kuheshimu tamaduni, Ambindwile pia ni Wakili Binafsi wa Mtwa wa Wahehe, Adam Mkwawa wa Pili, nafasi ambayo inaakisi heshima aliyoijenga ndani ya jamii.
Akihojiwa kuhusu hatua yake ya kuchukua fomu, Ambindwile alisema:
“Nimechukua fomu kuomba ridhaa ya chama changu kiniteue kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huu mkuu. Nia yangu ni kutekeleza Ilani ya Chama kwa mwaka 2025 hadi 2030, kwa msingi wa haki, weledi na utumishi uliotukuka kwa wananchi.”
Wakili huyo pia ni mjumbe wa bodi mbalimbali za taasisi na mashirika, na ni miongoni mwa wakurugenzi waliothibitishwa kitaifa na Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT).
Kwa weledi, maadili, na historia yake ya kutetea wanyonge, kuwania kwake ubunge kunazua mjadala mpya juu ya nafasi ya wataalamu wa sheria katika siasa, huku jina lake likiwa gumzo miongoni mwa wakazi wa Iringa Mjini kama alama ya matumaini mapya.

