Wakili anayehudhuria mkutano TLS afariki ghafla
DODOMA; WAKILI Maria Pengo(36) amefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia leo kwa shambulio la moyo(heart attack).
Maria alikuwa miongoni mwa mamia ya mawakili waliofika mkoani Dodoma kushiriki mkutano mkuu wa mwaka unaokwenda sambamba na uchaguzi mkuu wa The Tanganyika Law Society (TLS).
taarifa zilizosambazwa kwa mawakili zinasema kuwa mwili wa wakili huyo utasafirishwa leo jioni kwenda nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.
Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Renetha Mzanje amethibitisha kupokelewa kwa mwili wa wakili huyo saa 7 usiku wa kumkia leo.
Naye mjomba wa marehemu, Julius Msengezi, amesema Maria alianza kupata changamoto saa tatu usiku na kukimbizwa hospitali ili kuokoa uhaki wake na alifariki dunia saa 7 usiku.
“Kwa sasa tunapeleka mwili wa marehemu nyumbani kwake Dar es Salaam na baadaye tutasafirisha mwili kuelekea Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa kwa ajili ya kumpumzisha,” amesema.
Naye Rais wa TLS anayemaliza muda wake, Sungusia Harold, amesema jambo la kufiwa na mwananchama wakati wa mkutano halijawahi kutokea, hivyo hawana mwongozo kuhusu suala hilo.
Soma pia: TLS yashauriwa kusimamia haki na amani
“Hatuna kanuni inapotokea tukio kama hili, hivyo tunatumia busara pekee. Pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Dk Eliezer Feleshi) amepata taarifa hizi na atakuja kuungana nasi kumuaga mpendwa wetu,” amesema.
View this post on Instagram
Mamia ya mawakili wanaohudhuria mkutano huo walitumia fursa ya kusimama kwa mkutano kumuaga Maria shughuli iliyofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete. Uchaguzi wa TLS unatarajiwa kufanyika kesho.