Wakulima mil 1.8 wasajiliwa mbolea ya ruzuku

mbolea

ZAIDI ya wakulima milioni 1.85 sawa na asilimia 25 ya wakulima wote wanaokadiriwa kufi ka milioni saba nchini, wamesajiliwa katika programu ya kidijiti ya M-Kulima inayowawezesha kupata mbolea ya ruzuku.

Idadi hiyo ni kati ya wakulima 2,579,590 walioandikishwa kwenye madaftari ya usajili katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuingizwa katika mfumo. Utaratibu ambao unaendelea nchini kote kwa lengo la kuhakikisha wakulima wote wanasajiliwa.

Akizungumza na HabariLEO katika mahojiano maalumu mkoani Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk Stephan Ngailo alisema hadi Oktoba 20, mwaka huu jumla ya wakulima waliosajiliwa kwenye mfumo wa kidijiti ni 1,853,185.

Advertisement

Wakati wakulima hao wakiendelea kusajiliwa katika maeneo yao, hadi sasa mikoa yote 26, Tanzania Bara imeshaanza kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima waliojisajili na maeneo ambayo msimu wa kilimo umeanza, wakulima wameeleza kufurahia ruzuku hiyo.

Dk Ngailo alisema ili kuhakikisha wakulima wanasogezewa mbolea hiyo karibu na maeneo yao, zipo kampuni kubwa za mbolea 33, nchini na mawakala zaidi ya 2,065 wanaosambaza mbolea hiyo kwa wakulima ili kurahisisha upatikanaji wake.

“Tunaendelea kutoa rai kwa kampuni na mawakala wa pembejeo na mbolea kuhakikisha wanasogeza huduma ya mbolea karibu na wakulima, hadi sasa mawakala waliosajiliwa wa mbolea nchini wapo 2,065,” alisema Dk Ngailo.

Alisema mikoa yote nchini ina mawakala wa mbolea na serikali inaendelea kuhamasisha kampuni za mbolea kutafuta mawakala wa kusambaza mbolea kuondoa upungufu kwenye maeneo yenye tatizo hilo Dk Ngailo aliwataka mawakala wa mbolea za ruzuku kuongeza watendaji ili kuweza kuhudumia wakulima wengi zaidi wanaofika kununua mbolea hizo kwani mfumo unaotumika kuuza mbolea ni mpya na wafanyabiashara wanakwenda taratibu kwa kuwa hawajauzoea.

Aliwashauri mawakala hao waongeze watumishi hatua itakayosaidia kupunguza foleni ya wakulima kwenye maghala na maduka ya mbolea. Alisema msimu ujao changamoto hiyo itapungua kwa kiwango kikubwa.

Dk Ngailo aliwataka viongozi kwenye halmashauri mbalimbali nchini kuhimiza maofisa kilimo na wakulima kujisajili ili kunufaika na mbolea ya ruzuku.

Alishauri wakulima walio kwenye vyama vya ushirika (Amcos) kununua mbolea kupitia viongozi wao kwa kuzingatia taarifa walizowasilisha wakati wa usajili.

Akizungumzia kiwango cha mbolea kilichopo nchini, Dk Ngailo alisema hadi Oktoba 20, mwaka huu nchi ilikuwa na tani za mbolea 284,031 na shehena mpya ya tani 55,000 itawasili muda wowote kuanzia sasa nchini. Hivi karibuni, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisisitiza wakulima nchini kuendelea kujisajili kunufaika na mbolea ya ruzuku. Alisema hadi sasa wakulima waliosajiliwa ni milioni 1.8 sawa na asilimia 25 ya wakulima wote nchini.

“Tangu tuanze kusajili wakulima miezi miwili iliyopita, tumefanikiwa kusajili asilimia 25 ya wakulima, lengo letu ni kusajili wakulima wote nchini ifikapo Desemba mwaka huu, wakulima waliopo nchini wanakadiriwa kufika milioni saba,” alisema Bashe.

Serikali ilitenga Sh bilioni 150 kugharimia ruzuku ya mbolea nchini inayotolewa kwa wakulima wote kuwapunguzia makali ya bei. Mbolea zinazohusika katika ruzuku hiyo ni za kupandia, kukuzia kulingana na mahitaji.