Wakulima Regrow kuboreshewa umwagiliaji

KATIBU Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dk Hassan Abbasi amesema wakulima walio katika mradi wa kuboresha utalii Kusini (REGROW) wanaboreshewa miundombinu ya umwagiliaji kuwa ya kisasa ili maji wanayoyatumia yarejeshwe kwenye Bonde la Ihefu na Mto Ruaha Mkuu.

Dk Abbas amesema hayo mara baada ya kutembelea sehemu ya mradi huo katika skimu ya Madibira, Mbarali, Mbeya.

Amesema hatua hizo za uboreshaji si tu zimewasaidia wakulima pembeni mwa Hifadhi ya Taifa Ruaha na kuongeza mazao lakini tayari pia zimeonesha matumaini ya kuurejeshea uhai zaidi Mto Ruaha Mkuu ambao kwa sasa siku za kukauka kwa mwaka zimepungua.

Dk Abbasi ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi wa REGROW Madibira ni tafasiri kwa vitendo falsafa ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya “Kazi inaendelea” ya kuwapatia watanzania maendeleo kwa haraka.

Aidha Dk Abbasi ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi wa REGROW Madibira sanjari na kuboresha matumizi rafiki ya maji kwa wakulima wa mpunga ili maji yatiririke mto Mkuu Ruaha kwa uhifadhi endelevu wa Ikolojia na Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Ruaha unakwenda kusaidia upatikanaji wa maji ya uhakika katika Mradi wa Bwawa la kufua umeme la Mwl Nyerere.

“Mto Ruaha Mkuu ni tunu muhimu kwa hifadhi zetu ikiwemo Ruaha lakini pia unachangia asilimia 15 ya maji katika Mto Rufiji na hivyo ni uhai wa Bwawa la Nyerere”. Amesisitiza Dk Abbasi.

Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji Madibira, unaotekelezwa na Mkandarasi mzawa kampuni ya SkyLine, unaurefu wa takribani kilomita 13 na imekamilika kwa asilimia 95.

 

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button