Wakulima watakiwa kupima udongo
SONGWE; Momba. Wakulima wa mazao mbalimbali Wilaya ya Momba mkoani Songwe wametakiwa kupima afya ya udongo kujua upungufu wa virutubisho vilivyopo kwenye maeneo yao, ili waweze kutumia mbolea sahihi kulingana na upungufu wa virutubisho kwenye ardhi.
Mtafiti kutoka wizara ya Kilimo kituo Cha Utafiti (TARI) Ilonga Morogoro, Baraka Daniel amesema hayo katika ziara ya siku 14 ya watalaam wa kilimo na Mbunge wa Jimbo la Momba Condester Sichalwe.
Amesema matumizi ya mbolea pasipo kujua upungufu wa virutubisho vilivyopo kwenye ardhi husababisha wakulima kupata mavuno kidogo, kwa sababu hutumia mbolea kwa kukisia, ambapo huweza kutumia kidogo au kuzidisha tofauti na uhitaji.
“Kilimo bora chenye tija kinahitaji vitu vinne muhimu, ambavyo ni kupima afya ya udongo, kutumia mbegu bora ambazo tunazalisha sisi TARI kulingana na ukanda husika, kufuata kanuni bora za kilimo kama vile kuandaa shamba kwa wakati na kudhibit wadudu na kuwa na soko la uhakika, ambalo husimamiwa na serikal,” amesema Daniel.
Ofisa Kilimo Wilaya ya Momba, Robert Katenga amesema tayari serikali imenunua na kuwapatia kifaa cha kupimia udongo, hivyo kueleza kuwa wataanza kuzunguka kata zote 14 za Wilaya ya Momba, ili msimu wa kilimo unapoanza wakulima wajue mbolea ya kutumia katika ardhi wanayolima.
Mtalaam wa zao la mahindi kutoka kituo TARI Uyole, Julias Sanga amesema mkulima akijua afya ya udongo ni rahis kupata mavuno mengi kuanzia gunia 25 mpaka gunia 35 kwa ekari moja.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Momba Condester Sichalwe amesema lengo la ziara hiyo ni kuwapa fursa wakulima wa Momba, ambao hulima maeneo makubwa lakini hupata mavuno kidogo kutokana na kulima kilimo cha mazoea ambacho hutumia mbegu za asili.
“Nataka wananchi wa Jimbo la Momba tuwe matajiri kupitia kilimo, nataka wakulima tulime eneo dogo lakini tupate mavuno mengi ambayo tukiuza tutafanikiwa kujenga nyumba nzuri na kununua usafiri hasa pikipiki na kusomesha watoto wetu, ” amesema Condester.