Wakulima zao la mkonge kutumia bandari ya Tanga

SERIKALI imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kuwawezesha kiuchumi wawekezaji na wakulima wa zao la Mkonge Ili kuitumia bandari ya Tanga kusafirisha bidhaa za mkonge kwenda nje ya nchi.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo amesema hayo wakati wa ziara yake pamoja na wadau wa zao hilo kutoka wilayani humo katika Bandari ya Tanga Ili kujionea maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali.

Amesema kuwa lengo ni kutumia fursa ya bandari kwa ajili ya kusaidia kusafirisha bidhaa zitokanazo na zao hilo Kwa urahisi kwenda nje ya nchi na kuitumia bandari hiyo Kwa ufanisi tofauti na hapo awali

“Wakati huu ambapo serikali inaendelea na uhamasishaji wa kilimo cha mkonge nilionao ni vema kuwaletea wakulima na wadau wa zao Hilo waweze kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika Bandari yetu lakini na jinsi huduma zilivyoweza kuboreshwa”amesema DC Mwegelo.

Naye Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha amesema maboresho ya bandari hiyo ambayo kwa sasa yamefikia asilimia 99.6 kadiri siku zinavyokwenda milango ya kibiashara inazidi kufunguka na wafanyabiashara kuonyesha nia ya dhati kuitumia bandari hiyo hatua ambayo itazidi kuchangia kuongezeka kwa pato la Taifa .

“Tumefurahushwa sana na ujio huu kwani tumeweza kujadili fursa na changamoto mbalimbali ambazo zinatokana na zao hili la Mkonge kupitia bandari yetu ya Tanga tunawaahidi baada ya maboresho yaliyofanyika katika bandari yetu sasa hivi wadau wetu wazalishaji wote wa zao la Mkonge waje kutumia bandari yetu ya Tanga na zile gharama kubwa ambazo zimekuwa zikisababisha wakimbie Sasa hazipo tena”amesema Mrisha.

Habari Zifananazo

Back to top button