Walimu, wanafunzi watumia choo kimoja Butiama

WALIMU wa Shule Shikizi ya Kijiji cha Nyabange, Kata ya Nyankanga, Wilaya ya Butiama mkoani Mara wanatumia choo kimoja na wanafunzi kwa upungufu wa vyoo.

Serikali ya Kijiji hicho inahutuhumiwa kuchelewesha utatuzi wa kero hiyo, licha ya wananchi kuchimba shimo lingine la choo na kuchanga fedha za ujenzi.

“Tuna wanafunzi zaidi ya 200 kuanzia chekechea mpaka darasa la pili, ambao awali walitumia mlango mmoja kuingia chooni, tukawatenga kwa sasa wavulana wanatumia  matundu mawili na wakike  tunatumia pamoja matundu  yaliyosalia,” alisema Mwalimu Grace Magesa, ikimaanisha tundu moja linatumiwa na watu wasiopungua 40.

Alisema jamii ipo tayari kujitolea tatizo ni viongozi wao, kwamba ujenzi wa shimo unaosimamiwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Agostino Simon ulianza mwishoni mwa Mei, 2022 lakini ulisimama baada ya siku tano.

“Nilisikia fundi alipata kazi Meatu, nilimpigia simu akasema atakuja kumalizia wiki ya sensa,” alisema Magesa.

Kero hiyo ni miongoni mwa zilizoibuliwa kwenye mkutano wa hadhara, viongozi wa vitongoji mpaka wilaya wakisikiliza kero za wanakijiji ili kuzitatua.

Diwani wa Kata hiyo, Jacob Shasha alisema kila mvuvi anachangishwa Sh 5,000 kila mmoja kusaidia ujenzi huo, lakini Mtendaji wa Kijiji hicho, Husna Juma alinyimwa taarifa.

Mkazi wa Nyabange, James Surera, alitaka Juma awaeleze kinachoendelea na ikiwa kitabu kinachotumiwa kuchangisha fedha hizo ni cha serikali kilitokaje ofisini kwake.

Juma alikiri kushiriki kuhamasisha wadau kuchangia ujenzi huo na alisikia kuwa wavuvi wanachangishwa fedha, lakini alipompigia simu Moshi (mchangishaji) kuomba taarifa ya mapato hayo alimtaka amuulize aliyempa kitabu(Simon), kwamba hata kitabu hakuwa akijua kilikuwa cha aina gani.

“Naamini baada ya mkutano huu, Simon atanipa taarifa zote na nitazileta kwenye taarifa ya mapato na matumizi katika    mkutano mkuu wa kijiji,” alisema Juma.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Simon alisema majibu ya Juma yalitokana na jinsi alivyoulizwa, lakini baada ya kuhamasisha wadau, walikubaliana kiongozi wa wavuvi, Moshi akusanye Sh 5,000 kwa kila mvuvi na siku waliyohitaji kitabu, hakuwa kazini hivyo alimuomba akachukue kitabu kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mushandwa, Magesa Chacha na kumpatia Moshi.

Licha ya kutokumbuka namba ya kitabu hicho, Simon alisema ni cha serikali, ambavyo hutolewa na halmashauri, chenye risiti 50 na kufuatia yaliyotokea kwenye mkutano, alimuagiza Moshi akabidhi fedha zilibakia na kitabu kwa Juma.

Jumla Sh 220,000 zilichangwa na wavuvi hao wa eneo la Mwigaraganja na sehemu yake ilitumiwa ambapo baadhi zilitumiwa kumlipa fundi.

Alisema ujenzi wa shimo hilo lenye urefu wa futi 10 na upana futi nane, umebakiza futi tatu kukamilishwa na kwamba fundi hakuwa kazini kwa sababu ya kuuguliwa na alizungumza naye akaahidi kumalizia wakati wowote kuanzia juzi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button