Walimu wapewa mafunzo ya Kingereza Iringa

IRINGA: WALIMU wa shule za msingi Manispaa ya Iringa wameanza kupatiwa mafunzo ya siku tatu kuhusu mbinu mpya ya kufundisha Kiingereza kwa kutumia mfumo wa Jolly Phonics.

Mfumo huo unaolenga kuwasaidia wanafunzi wa darasa la kwanza kujifunza kusoma na kuandika kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza katika mafunzo hayo yanayofanyika katika Shule ya Msingi Mapinduzi, Mratibu wa Mafunzo kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Stephen Mwashihara amesema mpango huo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Elimu kupitia TET katika kuboresha ufundishaji wa somo la Kiingereza kuanzia ngazi ya awali.

“Maboresho haya ni mahsusi kwa shule zinazotumia Kiswahili kufundishia, lakini sasa tunaanza kufundisha Kiingereza kuanzia darasa la kwanza. Kupitia mfumo huu wa Jolly Phonics, tunawajengea walimu uwezo wa kutumia mbinu za sauti, ishara na picha kumfundisha mwanafunzi namna ya kutamka na kuandika maneno kwa usahihi,” amesema Mwashihara.

Jolly Phonics ni mbinu ya kufundishia Kiingereza inayojikita katika mafundisho ya sauti 42 za msingi za lugha hiyo, ambapo mwanafunzi hujifunza kwa kutumia michezo, nyimbo na hadithi, hivyo kumuwezesha kuelewa lugha kwa haraka na kwa njia ya kufurahisha.

Tayari nchi kadhaa barani Afrika kama Kenya, Uganda, Nigeria na Afrika Kusini zinatekeleza mpango huu kwa mafanikio makubwa.

SOMA ZAIDI: Walimu wa masomo ya sanyansi, hisabati wapigwa msasa

Kwa upande wa Tanzania, mikoa ya Iringa, Tabora, Rukwa na Arusha imenufaika na mpango huo unaolenga kuboresha viwango vya ufaulu wa somo la Kiingereza, ambalo kwa muda mrefu limekuwa changamoto kwa wanafunzi wengi.

Miongoni mwa walimu walioshiriki mafunzo hayo ni Mwalimu Etenes Msimika kutoka shule ya msingi Mshikamano, ambaye amesema mafunzo hayo yamempa mwanga mkubwa wa namna bora ya kufundisha somo la Kiingereza kwa watoto wadogo.

“Awali tulikuwa tunawafundisha watoto Kiingereza bila mbinu rafiki, lakini kupitia Jolly Phonics nitaweza kuwafundisha wanafunzi wangu kwa kutumia sauti na picha, jambo ambalo litawasaidia kuelewa na kupenda somo,” amesema Msimika.

Naye Mwalimu David Mkoma wa shule ya msingi Ugele amesema maarifa aliyoyapata yataenda kubadilisha kabisa namna anavyofundisha darasa la kwanza.

“Mafunzo haya yametufungua macho. Sasa nitakuwa na uwezo wa kutumia mbinu shirikishi zaidi, ambapo watoto watashiriki kikamilifu na siyo tu kusikiliza,” alisema Mkoma.

Mpango huu unatarajiwa kuongeza ufaulu wa somo la Kiingereza na kuondoa changamoto ya wanafunzi kufika ngazi za juu za elimu kutokuwa na uwezo wa kuandika wala kuzungumza lugha hiyo kwa ufasaha.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button