Walimu wasio na ajira waitwa Dodoma

SERIKALI imesema ipo tayari kukutana na viongozi wa vijana waliojitambulisha kuwa ni Umoja wa Walimu Wasio na Ajira (NETO).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewaita vijana hao ofisini kwake Dodoma wazungumze.
Simbachawene alisema hayo Morogoro juzi alipokagua timu inayosimamia mchakato wa ajira za ualimu katika Kituo cha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
“Nimesoma makala yao yenye kichwa cha habari ombi la wahitimu wa ualimu vyuo mbalimbali nchini kati ya mwaka 2015 hadi 2023 kwa serikali, andiko lao ni zuri na linaeleweka ingawa linahitaji ufafanuzi zaidi, hivyo ninatoa wito kwa vijana hao kuja ofisini Dodoma kwa mazungumzo,” alisema.
Simbachawene alisema aliwasiliana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa kuhusu jambo hilo.
“Walinieleza kuwa na wao wameuona na kwamba tayari wamekubaliana kushiriki kwenye mazungumzo hayo wakati kundi hili litakapokuwa tayari,” alisema.
Simbachawene alisema Serikali ya Awamu ya Sita inazingatia misingi ya falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya).
Ameagiza makatibu wakuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Katibu Mkuu Tamisemi na Katibu Mkuu wa ofisi yake wawasiliane na viongozi wa umoja huo ili wakutane sehemu ambayo wao wataridhia Dar es Salaam au Dodoma.
“Wasiogope kujitokeza kukutana na serikali yao na si jambo zuri kuendeleza mogogoro kupitia mitandaoni kwani serikali haifanyi kazi kujibu hoja kupitia mitandaoni bali ni kwa majadiliano,” alisema Simbachawene.
Ameipongeza timu inayosimamia mchakato wa ajira za ualimu kwa namna wanavyofanya kazi hiyo kwa uadilifu na ufanisi.
Simbachawene alisema kuanzia Januari 14 hadi Februari 24 mwaka huu, serikali kupitia Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (Utumishi), Ofisi ya Rais- Tamisemi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Wizara ya Afya; Tume ya Utumishi wa Walimu, ofisi za wakuu wa mikoa yote na wataalamu katika taasisi za umma, wanafanya kazi ya usaili wa kada za ualimu.
“Usaili huu una lengo la kujaza nafasi 14,648 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu nchini,” alisema.
Msimamizi wa kituo cha SUA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hilda Kabissa alisema wanasimamia usaili wa aina tatu ukiwemo wa kuandika, wa vitendo na wa mahojiano ya ana kwa ana kwa kuzingatia mahitaji ya kada au nafasi inayotakiwa kujazwa.



