Walimu watatu wasota jela makosa ya mitihani
WALIMU watatu nchini Uganda; Robert Mubiru, Wenecelaus Twongereirwe na Vincent Atukwase wanaokabiliwa na kesi ya kuvujisha mtihani nchini humo wameendelea kusalia rumande hadi Januari 9, 2023 baada ya ombi lao la dhamana kutosikilizwa.
Uamuzi huo ulitolewa na hakimu, James Bwambale baada ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Masaka, Sylvia Nvanungi anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo mahakamani hapo.
Inadaiwa kuwa Novemba 9, mwaka huu, walimu hao kwa kushirikiana na watu wengine walihusika katika kuvujisha Mitihani ya Kumaliza Elimu ya Msingi (PLE) kwa kuipiga picha na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya uamuzi Ofisa Mwandamizi wa Sheria wa Baraza la Mitihani la Uganda (UNEB), Annet Kemale, alisema Baraza liko tayari kuendelea na kesi hiyo na kuongeza kuwa Uneb imejitolea kupambana na makosa ya mitihani nchini humo.
“Hakimu ambaye alipaswa kushughulikia ombi la dhamana hakuwepo na katika hali kama hiyo, hakuna kitu kinachoweza kutokea zaidi ya kurudishwa rumande,” alisema.
Sheria ya Baraza la Mitihani Uganda inaharamisha usaidizi wa makusudi au wa uzembe au kusababisha mtahiniwa yeyote kupata karatasi za mitihani.
Iwapo watapatikana na hatia, wahusika watatozwa faini isiyozidi Sh milioni 40 au kifungo kisichozidi miaka 10 au vyote kwa pamoja.
Vilevile, adhabu ya makosa ya mtihani imeongezwa kutoka Sh 50,000 au kifungo cha miaka miwili jela hadi kufikia faini ya Sh milioni 10 au kifungo cha miaka mitano jela au vyote kwa pamoja kulingana na uzito wa kosa.