Waliopisha ujenzi soko kuu Bariadi kupewa kipaumbele

SIMIYU: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza serikali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu kuhakikisha wafanyabishara waliopisha ujenzi wa Soko Kuu la Bariadi wapewe vipaumbele kabla kuruhusu watu wapya.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi ameelekeza hayo leo Machi 9,2026 alipokagua mradi wa ujenzi wa soko hilo linalojengwa wilayani katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Ilielezwa mradi huo wa soko unajengwa kwa zaidi ya kiasi cha Sh bilioni 5.2 ukiwa ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa katika kifurushi ambayo inatekelezwa katika Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC) katika halmashauri hiyo.
Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Mjenzi ambaye ni Kampuni ya SIHOTECH Engineering Company Ltd na Global Multi-Contractor Company Limited ambaye alishinda zabuni na hadi sasa amefikia asilimia 25 ya utekelezaji wake.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Kihongosi amesema ametoa maagizo hayo kwa sababu CCM imejengwa katika misingi ya kuheshimu utu wa watu na kusimamia haki za wananchi.

“Nimetoa agizo lingine kwa viongozi wa serikali kuhakikisha wanasimamia haki na uwazi katika ugawaji wa vibanda na maduka ya soko hili. Wafanyabiashara waliokuwepo hapo awali wapewe kipaumbele cha kupata maduka mpaka wote wapate yanayobaki ndo wapewa watu wapya,” ameelekeza Kihongosi.
Ameongeza kwa kutoa rai kwa viongozi wa umma na chama kwamba haitapendeza kuona mtu mmoja hususani kiongozi anamiliki maduka mengi,yaani zaidi ya moja kwa lengo la kuyapangisha kwa wengine, akieleza halitakuwa sahihi na wamekataza kabisa hali hiyo.

“Wanaostahili kupata maduka wapewe kwa utaratibu mzuri, kwa haki na bila upendeleo wala kumonea mtu.Naamini jambo hili litasimamiwa vizuri na viongozi wetu wa mkoa, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama pamoja na Mkuu wa Mkoa na Wilaya, pia viongozi wa wilaya waliopo hapa,” amesisitiza Kihongosi.



