Waliopisha upanuzi uwanja wa ndege walipwa mil 700/-

NAIBU Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Ujenzi Dk Charles Msonde ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuwa zaidi ya Sh milioni 700 zimelipwa fidia kwa wananchi waliokuwa wamepisha eneo la upanuzi wa uwanja wa ndege uliopo eneo la Ibadakuli mkoani Shinyanga.

Dk Msonde amesema hayo jana mbele ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Vuma walipokuwa wakikagua eneo lililotengwa kwa ajili ya uwanja wa ndege na ofisi ambapo alieleza fedha hizo zililipwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 zaidi ya Sh milioni 500.

Advertisement

Msonde amesema baada ya wananchi kulalamika kuwa wamepunjwa mwaka 2024 serikali ilitoa zaidi ya Sh milioni 200 nakulipwa kama mapunjo yao kwenye fidia na imefanyika pia kwenye kuhamisha makaburi matatu yaliyokuwa ndani ya eneo la ujenzi huku mchakato mwingine ukiendelea kuhamisha mengine yaliyo nje ya ujenzi.

‘Kwa sasa mradi umefikia asilimia 75 kukamilika na mchakato umekwisha anza wa kuomba kibali kwaajili ya utumiaji wa uwanja wa ndege kwa kutimiza agizo kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,”amesema Dk Msonde.

Dk Msonde amesema mradi huo umetumia Sh bilioni 44.8 na wakati wa ujenzi umeweza kutoa ajira 240 za moja kwa moja hivyo ajira 230 sawa na asilimia 95 ni watanzania ikiwa wanawake ni 36 sawa na asilimia 15.

Vuma amesema ametoa ushauri waanze kufungua maeneo ya kufanyia biashara wakati wakiendelea kusubiri taratibu zingine huku wakimsisitiza mkandarasi kukamilisha asilimia 25 iliyobaki ndani ya muda uliopangwa.

“Niweze kuipongeza serikali kwa kuhakikisha imekamilisha fedha zote kwa mkandarasi ambaye amekuwa akisimamiwa na wakala ya barabara nchini (Tanroads) na baadhi ya maeneo muhimu yamekamilika kama barabara ya kuruka na kutua ndege,uzio wa usalama, barabara ya ndani ya kiwanja na kuingia uwanjani,”amesema Vumi.

Mbunge Viti Maalum, Santiel Kirumba kutoka mkoani Shinyanga amesema ukamilishaji wa uwanja huo utaleta faraja kwa wakazi wa mkoa huu kwani wafanyabiashara wengi wamekuwa wakienda mkoani Mwanza kupanda ndege nakuwalazimu kutumia gharama kubwa zaidi.

“Mkoa wa Shinyanga tulikuwa tunategemea uwanja wa ndege wa Kahama ambapo ndege inatua mara tatu kwa wiki nayo wakati mwingine inakuwa imejaa nakuwalazimu wafanyabiashara kukata tamaa tena kwa Kahama na kwenda mkoani Mwanza,”amesema Kirumba.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *