Waliozaa na waume za watu changamoto Pugu

TIMU ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia wilayani Ilala imebaini katika Kata ya Pugu baadhi ya wanawake wanazaa na waume za watu na kujihesabia haki kuwa nao ni wake halali ilihali ndoa ya awali ya mwanaume huyo haijavunjwa kisheria.

Hivyo mwito wao ni kuwa elimu iendelee kutolewa kwa wananchi ili wawe na ufahamu wa sheria ya ndoa na kutojihusisha na waume za watu kwa sababu ni kosa kisheria, lakini pia ni jambo lisilo na maadili katika jamii na linachangia uwepo wa migogoro isiyo na sababu za msingi.

Hayo yalibainishwa na Mratibu wa kampeni hiyo wilayani Ilala, Dk Baraka Mkami alipozungumza na HabariLEO kuhusu tathmini ya kampeni hiyo katika Kata ya Pugu ambayo ni moja ya kata 10 za Wilaya ya Ilala zilizolengwa wananchi wake wafikiwe na huduma hiyo inayotolewa bure.

“Tumebaini huku (Pugu) wanawake wengi wanazaa na waume za watu ambao wamefunga ndoa za Kikristo, na hao wanawake (hawara) wanajihesabia haki, wanapita kifua mbele hawana hadhari ilihali ni kosa kisheria,” alisema Dk Mkami.

Alisema ndoa ya kikristo ni ya mke mmoja na kuwa ili mwanaume aliyeoa ndoa hiyo aweze kuoa mwanamke mwingine ni lazima ndoa ya awali ivunjwe mahakamani kwa takala kutolewa, baada ya mahakama kupitia shauri husika na kujiridhisha na madai yaliyowasilishwa.

“Jamii ina changamoto na tatizo kubwa ni elimu, wanadhani mume kutengana na mkewe waliyefunga nae ndoa ya kikristo ndio kuachana na kuwa anaweza kuoa. Hapana, lazima kama shauri lifike mahakamani la kutaka kuivunja hiyo ndoa na lisikilizwe na kama lina mashiko ndio mahakama inafanya uamuzi na takala inatolewa,” alisema Dk Mkami.

Alisema ikishatolewa talaka ambayo ni cheti halali kisheria mgawanyo wa mali hufanywa kisheria ili kila upande upate stahiki yake na baada ya hapo mtalaka anaweza kuoa au kuolewa na ndoa yake kuwa halali.

“Lakini huku mtu ana ndoa ya kikristo halafu anapata mwanamke mwingine anaishi naye na kuzaa watoto, jambo ambalo ni kosa kisheria na haya ndio yanasababisha migogoro ya mirathi na ndoa,” alisema Dk Mkami.

Akizungumzia migogoro katika Kata ya Pugu na Mzinga ambako timu hiyo imeshapita kutoa huduma, Dk Mkami alisema wamepokea migogoro 54 katika maeneo hayo.

Alisema katika Kata ya Pugu walipokea migogoro 22 na minne kati ya hiyo imepata suluhu na mingine inaendela kupatiwa ufumbuzi na baadhi ya hiyo imeshauriwa kupelekwa kwenye vyombo vya maamuzi ya haki ngazi ya mahakama.

Alisema katika Kata ya Mzinga walipokea migogoro 32 na kati ya hiyo wamesuluhisha 14.

Dk Mkami alisema migogoro mingi inahusu ardhi, ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto na mirathi.

“Mfano kuna mgogoro mmoja tumeingilia kati kikao cha ndugu waliokaa kutaka kumdhulumu mjane nyumba waiuze bila kumshirikisha, timu yetu ikafika nyumbani na kusitisha uvunjifu huo wa sheria na kutaka ukoo ukae kwa kumshirikisha mjane na wafungue mirathi kwa njia halali ya kisheria,” alisema Dk Mkami.

Jana timu hiyo iliendelea kutoa huduma katika Kata ya Gongolamboto na leo ni zamu ya Kinyerezi kisha Tabata na kuhitimisha Chanika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button