Wamiliki bandari kavu watakiwa kuongeza ukubwa wa maeneo

DAR ES SALAAM: SERIKALI imeanza majadiliano na wamiliki wa bandari kavu pamoja na taasisi mbalimbali za umma kwa lengo la kuangalia namna bora ya kupanua na kuongeza uwezo wa bandari hizo, kufuatia kuongezeka kwa shughuli za Bandari ya Dar es Salaam.
Hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa mizigo bandarini, kuongeza ufanisi wa huduma za usafirishaji na uhifadhi wa mizigo pamoja na kuimarisha biashara na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Akizungumza leo Mei 8 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau kujadili uanzishwaji na uendeshaji wa bandari kavu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Salum, amesema wamiliki wa bandari kavu wanapaswa kuanza kufikiria kumiliki maeneo makubwa zaidi ili kuwezesha uondoshwaji wa mizigo kwa wingi kutoka Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema kwa sasa bandari hiyo inapokea wastani wa tani 110,000 za mizigo kwa mwezi ikilinganishwa na uwezo wake wa awali wa tani 28,000, hali inayoongeza umuhimu wa kuwa na maeneo makubwa ya kuhifadhi makontena.

Ameongeza kuwa asilimia 50 ya makontena yanayoingia bandarini husafirishwa kwenda nchi jirani huku asilimia nyingine ikibaki hapa nchini, jambo linaloongeza mahitaji ya bandari kavu zenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi mizigo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Usafiri Majini, Mussa Shashula, amesema kiwango cha mizigo bandarini kimeongezeka kutoka tani milioni 18 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 32 mwaka 2024/25, huku matarajio yakiwa kufikia tani milioni 34 mwaka 2025/26.

Amesema ongezeko hilo linaifanya serikali kuendelea kuweka mikakati ya kuboresha miundombinu ya bandari kavu ili kuendana na kasi ya ukuaji wa biashara na usafirishaji wa mizigo nchini.



