WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula amesema wamiliki wa ardhi nchini hivi karibuni wataanza kupokea bili za kodi ya pango la ardhi kupitia simu ya mkononi.
Dk Mabula amesema hayo leo April 11, 2023 wakati Makamu wa Rais Dk philip Mpango aliposimama kwa muda kuzungumza na wananchi wa Hungumalwa wilayani Misungwi mkoani Mwanza, wakati wa mwanzo wa ziara yake ya siku tatu mkoani humo.
“Ninapozungumza sasa mikoa kumi tayari imeunganishwa katika mfumo na tutaanza kupata bili zetu kupitia simu ya mkononi hivi karibuni, maana watu walikuwa wakihoji kama maji waliweza kwa nini ardhi wasiweze,” alisema Waziri Mabula.
Amesema kwa sasa kuna wataalamu 26 wanaboresha mifumo ndani ya wizara hiyo, lengo likiwa kuhakikisha mifumo ya wizara inaimarika katika masuala ya malipo, ili kuwawezesha mmiliki wa ardhi kuondokana na changamoto za ulipaji kodi ya pango la ardhi.
” Napenda niwahakikishie wanannchi wa Hungumalwa, Kwimba na wana Mwanza kwa ujumla kuwa zile kelele za ardhi zinaenda kuisha kwa sababu mama Samia ameiwezesha wizara,” alisema Dk Mabula.
Amesema Rais Dk Samia Suluhu Hassan amefungua nchi na kuhitaji kuwa na wawekezaji na kubainisha kuwa wawekezaji lazima wakute ardhi zipo na zimepangwa na kuwekwa kwa uwekezaji.
“Niwaombe katika kutenga maeneo ya uwekezaji lazima tuhakikishe yametambuliwa na yanamilikiwa, lengo muwekezaji akija asianze kuvutana na wananchi, halmashauri na serikali ya kijiji husika, iwe imefanya utaratibu wa kulitambua eneo na kumiliki,” alisema Dk Mabula.